HII NDIO SIRI YA MATOKEO MABOVU YA KIDATO CHA NNE...

Baadhi ya wanafunzi wakifanya mitihani ya Kidato cha Nne hivi karibuni.
Mitihani kusahau wenye welewa wa kawaida na wa chini, ndiyo siri kubwa ya kufeli kwa watahiniwa wa Kidato cha Nne katika matokeo yaliyotangazwa juzi Dar es Salaam, imeelezwa.
Hali hiyo ilitokana na maswali yaliyotolewa kuwa ya kitaalamu zaidi na hivyo kuwa magumu kwa wanafunzi wengi kiasi cha kushangaza hata shule zilizokuwa zikifanya vizuri zamani.
Akitoa maoni juu ya wanafunzi wengi wa kidato cha nne kufeli, Mwalimu wa Taaluma wa kundi la shule za Feza, alisema matokeo hayo yameishangaza shule hiyo na hivyo kukosa mwanafunzi mwenye ushindi wa alama saba kama ilivyozoeleka.
Mwalimu Simon Albert alisema jana, kwamba “maswali yalikuwa ya kitaalamu zaidi,” na kutoa mfano kwamba mbali na masomo ya Hisabati na Biolojia, masomo mengine yalikuwa magumu kwa kiwango cha wanafunzi wengi.
Alitoa mfano wa somo la Jiografia ambalo shuleni kwake-sekondari ya wavulana ya Feza-hakuna mwanafunzi aliyepata alama A isipokuwa mmoja aliyepata B. Alisema mtihani ulikuwa na mitego mingi.
Hata hivyo, Feza ilitoa washindi wawili wa kitaifa waliopata daraja la kwanza kwa alama tisa ambazo imesema haijawahi kukosa mshindi mwenye alama saba.
Matokeo hayo yameshangaza wengi na kutajwa kuwa janga na aibu kwa Taifa, hali ambayo wadau wametaka iundwe Tume kuchunguza mfumo wa elimu na wakati huo huo uwepo uwajibikaji wa viongozi wa juu wenye dhamana ya elimu.
Watu binafsi, taasisi, wanasiasa na wataalamu wa masuala ya elimu waliozungumza na gazeti hili jana, walitaka uandaliwe utaratibu kwa ajili ya  waliopata daraja la sifuri.  
Walisema wanafunzi 240,903 waliopata daraja hilo kuwaacha ni kupoteza hazina ya vipaji na utaalamu kwa kuwa kushindwa kwao hakumaanishi kwamba hawana akili isipokuwa ni mfumo mbovu wa elimu.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe pamoja na kutaka Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, naibu wake, Katibu Mkuu na Kamishna wawajibike kwa matokeo hayo, alitaka pia wizara hiyo ihamishiwe Ofisi ya Rais ili kunusuru sekta husika.
“Najua kuwa haina uhusiano wa moja kwa moja, maana matatizo ya elimu ni makubwa sana nchini. Lakini ni lazima kitu fulani kitokee ili kufanya mabadiliko. Uwajibikaji ni njia mojawapo inayoleta nidhamu na dharura katika utendaji kazi,” alisema Zitto.
Mbunge huyo aliendelea kusema: “Tumwambie Rais aichukue Wizara ya Elimu, kuwe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Elimu...tuwape masharti.”
Aliendelea: “Matokeo ya kidato cha nne ya namna hii; zaidi ya nusu ya wahitimu kupata sifuri  na takribani asilimia 90 kufeli kwa kupata daraja la nne na daraja la sifuri ni mwaka wa tatu sasa mfululizo… lazima uwajibikaji utokee”.
“Hawa watoto wanakwenda wapi?... ni vema tukope kuwekeza kwenye elimu, maana elimu ni hifadhi ya jamii. Elimu yetu ya sasa inazalisha matabaka kwenye jamii na ni hatari sana kwa uhai wa Taifa,” alisema  Zitto.
Alitaka mpango wa kujenga vyuo vya ufundi kila halmashauri ya wilaya uanze mara moja ili kunusuru watoto hao.  Kwa mujibu wake, katika bajeti kivuli mwaka 2011 walipiga  hesabu kwamba zinahitajika  Sh bilioni 720 katika kipindi cha miaka mitano ijayo kujenga vyuo hivyo kila wilaya.
Chama  cha NCCR-Mageuzi katika maoni yake, kilimwomba Rais Jakaya Kikwete kuunda Tume itakayojumuisha wataalamu waliobobea  katika  elimu ili kupata suluhu ya kuendelea kushuka kwa elimu kwa kuwa limekuwa janga la kitaifa.
Mwenyekiti wa Chama hicho, James Mbatia alitaka wadau wanasiasa, viongozi  na wengine kuweka kando itikadi za kisiasa na kutumia ujuzi wao kutetea sekta ya elimu, kwa kuwa ni suala la kitaifa lenye kumwathiri kila mmoja.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mbatia alisema Tume hiyo itatakiwa ilenge kuweka mikakati ya kuboresha elimu nchini.
“Sera ya elimu inayotumika sasa ni ya mwaka 1995 iliyosainiwa na Profesa Philemon Sarungi licha ya mabadiliko yote ya kidunia ambayo yamekuwa yakitokea,” alisema Mbatia. 
Washindi wa kitaifa walioongoza kwa kupata pointi tisa kutoka shule hiyo ya Feza ni Said Juma (17) na Jasper Kajule  (18).
Wakizungumza na mwandishi  wa habari hizi kwa nyakati tofauti jana, wanafunzi hao walisema baadhi ya maswali yaliyotoka kwenye mtihani yalikuwa  tofauti na waliyofundishwa.
Walitaka wanafunzi kutumia vizuri mitandao huku wakishukuru uamuzi wa shule hiyo kuzuia matumizi ya simu za mkononi shuleni.
Chadema kupitia kwa Waziri Kivuli wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Suzane Lyimo ilisema matokeo ya mwaka huu ni aibu kwa Taifa.
Alitaka Serikali ichukue uamuzi mgumu kudhibiti matokeo mabaya ili kuwezesha nchi kufanya vema katika soko la pamoja la Afrika Mashariki.
Mkurugenzi  Mtendaji wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Tanzania Coalition on Debt Development (TCDD), Hebron Mwakagenda alitaka hatua zichukuliwe haraka kuondoa hali mbaya ya elimu vijijini.
“Hotuba ya Waziri inaungana na TCDD kwamba hali ni mbaya zaidi vijijini kwa kila kitu … tunaomba hatua za haraka zichukuliwe ili kuondoa tatizo hilo,” alisema Mwakagenda.
Alisema shule ili iwe sekondari, vipo  vitu vya msingi kama madarasa, walimu, viwanja vya michezo, maabara na maktaba ambavyo ni lazima viwepo.
Utafiti wa TCCD  ambao taarifa yake iliwasilishwa hivi karibuni kwa wabunge, unabainisha kuwapo ongezeko kubwa la wanafunzi katika shule hususan za kata bila kuzingatia miundombinu ya mabweni, madarasa, vyoo, vitabu na walimu.
Katika uwiano baina ya walimu na wanafunzi ambacho ni kigezo muhimu katika kupima ubora wa elimu, utafiti unaonesha lipo tatizo kubwa. Kwa mfano utafiti huo ulibaini wilayani Kiteto, ipo shule moja ya sekondari ambayo mwalimu mmoja anahudumia wanafunzi 1,180.
Wakati uwiano wa kitaifa ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 35, utafiti uliofanyika katika wilaya saba ukihusisha sekondari 65 za kata, unaonesha wastani wa uwiano Kiteto ni 1:72, Iramba (1:67), Lindi (1:31) na  Kibaha (1:28).

No comments: