ALBINO WA MIAKA SABA AKATWA MKONO AKITOKA SHULE RUKWA...

Matukio ya ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi, yameendelea kushamiri mkoani Rukwa ambako siku moja baada ya jeshi la polisi kufukua mkono wa mwanamke albino uliokuwa umezikwa porini, watu wasiojulikana wamemfanyia unyama albino mwingine mtoto kwa kumnyofoa mkono wake mmoja na kutokomea nao kusikojulikana.
Mtoto huyo mwenye umri wa miaka saba, Mwigulu Matomange Magessa, ameripotiwa kushambuliwa na vijana watatu waliovaa `Kininja’ na kuunyofoa mkono wake wa kushoto.
Hayo yamethibitishwa na Diwani wa Kata ya Milepa,  Apolinary Macheta akisema tukio hilo lilitokea juzi saa kumi na moja  jioni  wakati  Mwigulu ambaye  anasoma darasa la kwanza katika Shule  ya Msingi Msia katika Kata  ya Milepa, Bonde la Ziwa Rukwa wilayani Sumbawanga  akirejea nyumbani Msia Mashambani  akiwa ameongozana na kundi la  wanafunzi  wenzake.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Peter Ngusa alipotafutwa kwa simu  kuelezea kadhia hiyo, ilielezwa kuwa hayupo ofisini tangu juzi usiku akiongoza msako dhidi ya watu waliofanya unyama huo.
Lakini diwani Macheta ameendelea kusema kuwa, hali ya Mwigulu bado ni mbaya kwani alipoteza damu nyingi na hatimaye kupoteza fahamu kabla ya kufikishwa katika zahanati ya Mtowisa katika Bonde la Ziwa Rukwa wilayani hapa.
Akisimulia zaidi, Macheta alisema  pamoja na kupiga kelele hawakuweza kupata msaada kutokana na mazingira ya eneo husika.
Kijiji  cha Msia  kimegawanyika  sehemu mbili 'Msia Center'  na 'Msia mashambani’.
Kwa mujibu wa diwani huyo  watoto  walipofika  kwa wazazi  wa  kule Msia mashambani  waliwasimulia  mkasa  uliowakuta  ndipo  ulipoanza msako  mkali wa kumtafuta mtoto Mwigulu  na kumkuta akiwa  mashambani na  huku mkono  wake mmoja ukiwa  umenyofolewa  na kumkimbiza  katika zahanati  ya  kijiji  cha jirani  cha Mtowisa ambapo  amelazwa  kwa  matibabu.
Ingawa Kaimu Kamanda  wa Ngusa  hakupatikana kwa simu, habari kutoka ndani ya jeshi hilo mkoani hapa zinathibitisha kutokea  kwa tukio  hilo  ambapo  hadi sasa  hakuna  yeyote  aliyekamatwa.

No comments: