WAUMINI WA KKKT WASHINDWA TENA KUSALI...

Waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Mtaa wa Themi jana walisusa tena ibada ya Jumapili na kugeuza muda wa ibada kuwa wa vikao vya kujadili michango ya ujenzi wa Kanisa.
Kabla ya uamuzi huo, waumini hao walipanga kuandamana lakini Msaidizi wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Solomoni Massangwa, alifanikiwa kuzima maandamano  hayo baada ya kuwaangukia waumini hao.
Tofauti na maandamano ya wiki iliyopita, maandamano ya jana yalikuwa dhidi ya kauli za Askofu Massangwa   kushindwa  kukubaliana na hoja zao, ikiwemo kutaka kujua mapato na matumizi ya harambee na sadaka za miaka miwili iliyopita kwa ajili ya ujenzi wa kanisa hilo.
Jumapili ya Januari 20, waumini hao waliandamana kwenda ofisi ya Mchungaji Kiongozi Larorya wa kanisa hilo, wakimtuhumu kukataa kueleza fedha za harambee za ujenzi wa kanisa hilo zilipo.
Katika jitihada za kuzima mgogoro wa kanisa hilo, juzi kikao cha kamati zote zilikutana lakini kikao hicho kilileta jazba na hasira, baada ya Askofu Massangwa kuwaeleza wajumbe wa kamati hizo kuwa hawana mamlaka ya kujua mapato ya harambee na sadaka za ujenzi wa kanisa.
Kutokana na hoja hizo, waumini hao walipanga kuandamana jana pamoja na wajumbe wa kamati zote wakiwa wamebeba vifaa vyote vya ujenzi na kuvirundika katika ofisi ya Mchungaji Larorya.
Baada ya kupata taarifa za maandamano, Askofu Massangwa alitinga katika Kanisa la Mtaa wa Themi saa 11.30 alfajiri jana na kuwaomba radhi waumini wa kanisa hilo na kamati zake zote.
Alipofika katika Kanisa hilo alfajiri, alikutana na  mabango mbalimbali ya waumini yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali dhidi ya ufisadi unaodaiwa kukithiri katika Kanisa hilo.
Baada ya kukuta mabango hayo, Askofu Massangwa ambaye aliwahi kunusurika kipigo cha waumini,  aliwaomba radhi na kutoa ombi la pili la kuwataka wasiandamane, baada ya kuwakubalia hoja zote
walizotoa bila ya masharti yoyote.
Baada ya kukubaliana kutoandamana, Askofu huyo alitaka waumini kusali kwanza kabla ya kuzungumza.
Hata hivyo, ombi hilo lilipingwa vikali na waumini na wajumbe wa kamati zote ambao walisikika wakisema  ‘’leo hakuna  kusali hapa mpaka tuzungumze.” 
Habari zilisema kutokana na hali hiyo, Massangwa aliwataka wajumbe wa kamati zote. Wazee wa Baraza la Kanisa hilo pamoja na waumini kuingia kanisani na kuanza mazungumzo yaliyochukua saa nne.
Mazungumzo hayo yalisababisha ibada mbili za kila siku za Kanisa hilo, kuahirishwa.
Mtoa habari wetu alisema waumini walianza kwa kumshambulia moja kwa moja Mchungaji Larorya kuwa ni mbinafsi na asiyetaka kushauriwa na anataka kufanya kila kitu mwenyewe bila kushirikisha kamati zote na hata wazee wa kanisa hilo.
Alisema kuwa Larorya alituhumiwa pia kuchukua fedha za harambee na sadaka kwa ujenzi wa kanisa kwa zaidi ya miaka miwili na nusu bila kufanyia kazi na kibaya zaidi kamati zote na hata ile ya ujenzi haijui ni kiasi gani kimepatikana na kimetumika kiasi gani.
Habari zilisema waumini na wajumbe wa kamati walitoa maneno makali na kumtahadharisha Msaidizi wa Askofu kuacha mara moja kumkumbatia Mchungaji huyo kwani hali inaweza kuchafuka ndani ya kanisa hilo.
Mtoa habari mwingine alisema baada ya kuona hali hiyo, Massangwa alikubaliana na hoja hizo na kuwaambia waumini na wajumbe wa kamati zote kuwa atamwagiza Mchungaji Larorya kuandaa mahesabu yake yote ya harambee na sadaka kwa muda huo na kuzisoma kanisani hapo mwezi ujao katikati.
Askofu Massangwa pia anadaiwa aliwasifu baadhi ya watu walioleza hoja na kusema kuwa hoja zao karibu zote zina msingi ndani yake kwani muumini ama mjumbe wa kamati hawezi kuchangia kitu bila kujua matumizi yake kwani hiyo haiwezi kuingia akilini.
Alisema pia Mchungaji Larorya anapaswa kushirikiana na kamati zote kwani huo ndio utaratibu wa utendaji kazi wa uwazi na ukweli.
"Sasa si tumemaliza kikao na kila kitu kimekwenda sawa sasa naomba kila kitu kiwe wazi na kama kuna shida naomba muniite mara moja na sio kuandamana na kutoa katika gazeti moja ambalo kila kukicha kinatoa habari hizi,’’ alinukuliwa Massangwa.

No comments: