WASICHANA WATANO WAMIMINIWA RISASI KWA KUELIMISHA WANAWAKE...

Malala Yousufzai
Wanawake watano nchini Pakistan wameuawa kikatili na wanamgambo wa Kiislamu waliowekwa maalumu kuzuia wanawake na wasichana kupata elimu.
Waliuawa katika uvamizi uliofanya Siku ya Mwaka Mpya katika gari lililowabeba kuwapeleka majumbani kutoka kazini kwenye kituo cha jamii na shule ya msingi katika eneo lililoko kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo.
Walimu hao na wafanyakazi wawili wa afya - mmoja mwanaume na mmoja mwanamke - waliuawa jana mchana katika jimbo lisilopenda mabadiliko la Khyber Pakhtunkhwa la Pakistan.
Ilikuwa katika mkoa huu ambapo Oktoba mwaka jana askari wa Taliban alimpiga risasi kichwani msichana Malala Yousufzai mwenye miaka 15 kwa kuwapinga wanamgambo hao na kuhamasisha elimu kwa wasichana. Msichana huyo kwa sasa anaendelea vizuri nchini Uingereza anakopatiwa matibabu.
Shambulio hilo lilikuwa ni kukumbushia hatari wanazokumbana nazo waelimishaji na wafanyakazi wa kujitolea, hususani wanawake, katika eneo ambako wanamgambo wa Kiislamu mara kwa mara wanawalenga wasichana na wanawake wanaojaribu kupata elimu.
Wanamgambo wengi katika jimbo la Khyber Pakhtunkhwa wanapinga elimu kwa wanawake na wamelipua shule na kuua waelimishaji wanawake kama njia ya kuwazuia wasichana wasipate elimu.
Wafanyakazi hao walikuwa njiani kutoka kazini katika mji wa Swabi ambako walikuwa wakifanya kazi kwenye shule ya msingi na kituo cha afya. Askari waliokuwa kwenye pikipiki wakawamiminia risasi kwa silaha zao za kisasa, alisema Javed Akhtar, mkurugenzi mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la Support With Working Solutions.
Shirika hilo linaandaa programu katika sekta za elimu na afya na kuendesha shule ya msingi na zahanati ndani ya kituo cha jamii mjini Swabi, alisema.
Mkuu wa polisi wa Swabi, Abdur Rasheed alisema wengi wa wanawake waliouawa walikuwa wa umri kati ya miaka 20 na 22. Alisema askari wanne wenye silaha ambao walitumia pikipiki mbili walivamia eneo la tukio na walikuwa bado hawajakamatwa.
Hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na tukio hilo.

No comments: