WANAOSHI KIGAMBONI SASA KUJENGEWA MAGHOROFA...

Kivuko cha mv Kigamboni ambacho ndio tegemeo lao kuu la wakazi wa Kigamboni katika usafiri.
Eneo la Kigamboni, Dar es Salaam limeondolewa katika utawala wa Manispaa ya Temeke na kuundwa muundo mpya wa Wakala wa Kusimamia Uendelezaji wa Mji wa Kigamboni (KDA) itakayoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji.
Wakala huyo ametengewa bajeti inayojumuisha fidia ya Sh trilioni 11.5, fedha zitakazotolewa na Serikali na sekta binafsi kwa miaka 20  mpaka mwaka 2032 na kwa mwaka huu, Sh bilioni 60 zimetengwa kuanzisha wakala huyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana na waandishi wa habari kuhusu uendelezaji wa mji huo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alisema utajengwa nyumba za kisasa na utakuwa na wakazi zaidi ya 400,000 wakati kwa sasa kuna wakazi 80,000 tu.
Pia wakala huyo atakuwa na wakurugenzi sita ambao watakuwa wakuu wa idara huku ikisimamiwa na Bodi na Baraza la Ushauri ambalo litakuwa na wajumbe wanaowakilisha wadau wote hususan wabunge na madiwani wa eneo litakaloendelezwa na KDA.
KDA itasimamia uendelezaji wa mji mpya Kigamboni kama Mamlaka ya Upangaji Mji katika eneo lenye ukubwa wa hekta 50,934 na kuhusisha kata za Kigamboni, Tungi, Vijibweni, Mjimwema, Kibada, Somangila, Kisarawe II, Kimbiji na Pemba Mnazi.
Alisema nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji itashindaniwa kimataifa na kutoa nafasi kwa Watanzania walioshiriki kupanga miji mbalimbali nje ya nchi kama Dubai na Malaysia.
Pia  wakuu wa idara hao sita na nafasi nyingine, pia zitatangazwa na kushindaniwa huku wakishirikishwa wananchi kwa kutumia Baraza la Kigamboni ambalo litakuwa na madiwani na mbunge wa eneo hilo.
Akizungumzia fidia kwa wakazi wa eneo hilo la KDA, alifafanua  kwamba baada ya tathmini, wakazi hao watahamishiwa katika nyumba zitakazojengwa na wawekezaji wa kuendeleza mji huo.
Mpaka sasa kwa mujibu wa Profesa Tibaijuka, kuna Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) ambalo liko tayari kujenga nyumba 500, mwekezaji Dubai Farm, atajenga nyumba 5,000 na kampuni ya China itajenga nyumba 15,900 na wawekezaji wengine.
Alisema nyumba hizo zitakazojengwa ndizo watahamishiwa wakazi hao kwa kutumia fidia watakazokuwa wamepewa kwenye tathmini na zitakuwa kwa wananchi wenye vipato tofauti.
“Hivyo mkazi atapewa nyumba kulingana na thamani anayotaka na pesa yake ikibaki atapewa na ikiwa anahitaji nyumba ya gharama kubwa kuliko fedha ya fidia, kutakuwa na benki zitakazomkopesha na mkazi huyo kulipa taratibu,” alibainisha.
Aliongeza kuwa jambo la msingi ni kuhakikisha wakazi wote wa Kigamboni wenye nyumba wanapata makazi na kama kuna mkazi ana nyumba yake eneo lingine Dar es Salaam, atapewa fedha yake ya fidia.
Waziri alisema wanafanya hivyo kuepusha kuwapa fedha wakazi hao na kuzitumia vibaya na kisha kujikuta wakikosa makazi na kudai kuwa fidia ilikuwa ndogo.
Profesa Tibaijuka alisema mthamini wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameanza tathmini.  
Kuhusu huduma kama za shule na hospitali zilizoko Temeke, Profesa Tibaijuka alisema wataangalia jinsi ya kufanya wakati huu wa mpito.
Alisema kwa wenye hati za viwanja na ujenzi ambavyo awali vilitolewa na manispaa ya Temeke, sasa zitatolewa na KDA ili kujenga mji mpya wenye huduma zote muhimu.
Akizungumzia changamoto katika Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) aliwahakikishia wakazi wa Kigamboni kwamba hazitatokea kwao, kwani mchakato wa ujenzi umechukua muda mrefu kwa kupata ushauri wa wataalamu.
Profesa Tibaijuka alisema ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni umeshirikisha wadau wote wakiwamo wabunge, madiwani na wananchi.

No comments: