WAJUMBE WA KAMATI WAMSUSIA KIKAO ASKOFU KKKT...


Msaidizi wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, Mchungaji Solomoni Massangwa amekumbwa na wakati mgumu baada ya wajumbe wa kamati za Kanisa hilo mtaa wa Themi, Usharika wa Mjini Kati kumsusia kikao huku wakimtolea maneno makali.
Hasira za wajumbe hao zimeelezwa kutokana na kinachodaiwa kuwa Mchungaji Massangwa anawadharau na kumlinda mchungaji kiongozi wa usharika wa Mjini Kati, Mchungaji Titus Larorya.
Adha kama hii ni ya pili kumkuta Mchungaji Massangwa katika siku za karibuni, kwani akiwa Usharika wa Ngateu, Jimbo la Arusha Magharibi, aliponea chupuchupu kupigwa, lakini aliokolewa akipitia mlango wa nyuma wa Kanisa baada ya wazee wa Usharika huo na kamati kumjia alipoonekana kutosikiliza hoja zao za kutaka Mchungaji Philemoni Mollel arudishwe kazini.
Katika kikao cha jana kilichoanza saa 4 asubuhi, wajumbe wa kamati za Kanisa hilo mtaa wa Themi, waliitwa katika ofisi za Usharika wa Mjini Kati na kuelezwa kuwa hawana mamlaka ya kuhoji mapato ya harambee na sadaka za ujenzi wa Kanisa hilo na matumizi yake.
Maelezo hayo yalitokana na kilichotokea Jumapili iliyopita, ambapo wajumbe hao na waumini wa Kanisa la Themi waliandamana wakibeba vifaa vya ujenzi hadi ofisini kwa Mchungaji wa Usharika huo, Larorya, na kumshinikiza kutosali ndani ya Kanisa hilo mpaka watakapopewa taarifa za mapato ya harambee na sadaka za miaka miwili na nusu iliyopita.
Vyanzo vyetu vya habari vilidokeza kuwa baada ya kauli ya Askofu Massangwa kwa wajumbe hao aliowataka wasihoji mapato na matumizi ya harambee na sadaka za ujenzi, majibizano makali yaliibuka na wajumbe kutoka nje ya kikao na kusema leo maandamano makubwa yatafanyika tena.
‘’Kesho (leo) tunafanya maandamano tena, sasa tunabeba kila kitu cha Mchungaji Larorya kilichopo ndani hadi ofisini kwake mtaa wa Goliondoi maana sasa maaskofu wanalinda wachungaji mafisadi wanaokula fedha za waumini bila ya woga,’’ alisema mtoa habari wetu. 
Akizungumza na mwandishi mara baada ya kikao kuvunjika, Elibariki Mbise ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Vijana, alisema kitendo cha Askofu Massangwa kuwaita kimyakimya wazee wa baraza la mtaa wa Themi na kuzungumza nao kwa siri, kinaashiria ajenda ya siri za kuficha mambo.
Mbise alisema hakuna mwumini anayetaka kuvuruga amani ndani ya Kanisa kama baadhi ya viongozi wa Dayosisi wanavyodai, bali kinachotakiwa ni wachungaji kushirikisha wajumbe wa kamati ndani ya Kanisa hilo, kila kitu kinachopatikana kwa maslahi ya Kanisa na si kwa mtu mmoja.
Alisema baadhi ya wachungaji na maaskofu wanautafsiri tofauti mgogoro huo, kwani kila kitu kingekuwa wazi kwa kamati na waumini, hali hiyo isingekuwapo, lakini vificho ndivyo vinavyoliingiza Kanisa kwenye ufisadi mkubwa wa mali zake.
‘’Hapa wachungaji na maaskofu wanashindwa kuelewa kilio cha waumini na wajumbe wa kamati na wazee wa Kanisa juu ya usiri wa taarifa za fedha, kwani wao si wanaotoa ila fedha zinatolewa na waumini, sasa kwa nini wao wanashindwa kutoa taarifa hiyo?
‘’Ukitaka kujua unaambiwa huna mamlaka, sasa kwa nini nilichaguliwa kuwa mjumbe wa Kanisa? Nitasema nini kwa waumini kwa kuchanga fedha zao kwa miaka miwili na nusu?” Alihoji Mbise. 
Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Kanisa, Alphonce Marandu alisema wakati umefika Kanisa kufanya kazi za kukusanya fedha kwa uwazi na kushirikisha kamati zote, vinginevyo mgogoro uliopo unaweza kusababisha madhara makubwa ndani ya Kanisa.
Marandu alisema suala la kukusanya fedha za harambee kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa na kufanya mambo bila kushirikisha kamati ni hatari,  hivyo wachungaji na maaskofu wanapaswa kubadilika, kwani waumini wa sasa si wa miaka ili ya nyuma.
Alisema maandamano ya leo yako palepale ili kuwaonesha wachungaji kuwa sasa kutoa fedha bila kujua matumizi yake ni hatari hivyo wanapaswa kubadilika.
Kuibuka kwa tuhuma za kutafunwa fedha za ujenzi wa kanisa ni mwendelezo wa mambo mengi yanayoendelea kufichuliwa ndani ya Kanisa hilo, Dayosisi ya Kaskazini Kati iliyo katika hatari ya kufilisiwa mali zake ikiwa pamoja na hoteli ya kitalii ya Arusha Corridor Springs kutokana na deni la Sh bilioni 11.
Kutokana na deni hilo, uongozi wa Dayosisi ulisambaza waraka kwa waumini wa kutakiwa kila mmoja kuchangia Sh 20,000 ili kunusuru mali za Kanisa, jambo lililoibua mgogoro, kwani wengi walipinga huku wakitaka maelezo ya sababu za mradi huo na mingine ya Kanisa kushindwa kuzalisha faida, licha ya kuonekana kufanya vizuri kibiashara.
Miongoni mwa waliopinga alikuwa Mchungaji Mollel wa Usharika wa Ngateu aliyetaka wahusika wa kadhia hiyo wachukuliwe hatua; lakini akageukwa na kufukuzwa na kuvuliwa madaraka ya kutoa huduma za kichungaji katika Kanisa hilo nchini.
Uamuzi huo ulivuruga hali ya hewa ndani ya Kanisa, huku wengi wakimwunga mkono na kutishia kuacha kutoa ushirikiano kwa Dayosisi, ikiwa ni pamoja na kutopeleka asilimia 40 ya sadaka kama mchango wa maendeleo ya Dayosisi hadi atakaporejeshwa kazini na kuendelea na shughuli za kichungaji.
Hadi sasa Mollel hajarudishwa kazini, lakini vikao vya ndani vimeripotiwa kufanyika kwa lengo la kutafuta mwafaka.

No comments: