UVIMBE WA HILLARY CLINTON KICHWANI WAICHANGANYA FAMILIA...

KUSHOTO: Hillary Clinton. KULIA: Chelsea Clinton akiwa amechanganyikiwa.
Sura yake imejaa machungu, hili lilitokea wakati Chelsea Clinton akiondoka Hospitali ya New York Presbyterian juzi baada ya kumtembelea mama yake, Hillary, ambaye ana donge la damu katikati ya ubongo na fuvu lake.
Chelsea alikuwa wa kwanza kutoka ukoo wa Clinton kuwa kando ya kitanda cha mama yake baada ya kuwa amelazwa Jumapili iliyopita.
Mapema baada ya taarifa ya hali yake kusambaa, utitiri wa vyombo vya habari ulikusanyika nje ya hospitali hiyo na kupiga picha uso wa Chelsea uliokuwa na mashaka wakati akiondoka hospitalini hapo.
Rais wa zamani, Bill Clinton baadaye aliwasili katika hospitali hiyo kumtembelea mkewe, naye pia akiwa na hali ya mashaka usoni wakati aliponaswa akiendesha gari lake kuondoka hapo baada ya kukaa kwa muda mfupi.
Waziri huyo wa Mambo ya Nje anatarajiwa kukaa hapo kwa siku nyingine chache akitibiwa tatizo hilo ambalo madaktari waligundua wakati wa ukaguzi wa kawaida wa afya yake baada ya Hillary kuanguka na kubamiza kichwa chini wiki mbili zilizopita.
Katika taarifa juzi, madaktari walihakikisha hali hiyo haihatarishi maisha yake na kuhakikisha kwamba hakuathirika ubongo wake ama tatizo la upoozaji.
"Kwa vipengele vingine vyote vya uponaji wake, Waziri huyu anaendelea vizuri sana na tunahakika atapona kabisa. Yuko vizuri, akishirikiana na madaktari wake, familia yake na wafanyakazi wake," Dk Lisa Bardack na Gigi El-Bayoumi walisema kwenye taarifa hiyo.
Hillary mwenye miaka 65 alilazwa hospitalini hapo Jumapili iliyopita na kituo cha CBS kiliripoti kwamba madaktari wanataka kufuatilia afya yake kwa japo masaa mengine 48.
Chelsea alikuwa mwanafamilia wa kwanza wa Clinton kuonekana hadharani katika hospitali hiyo.
Chelsea mwenye miaka 32, mwakilishi maalum wa NBC News, alionekana kuchanganyikiwa wakati akitoka hospitalini hapo - huku simu yake ikiwa mkononi. Alipuuza maswali kutoka kwa waandishi na kurejea tena ndani.
Madaktari wamesema Clinton alishambuliwa na virusi tumboni mapema Desemba na baadaye kuishiwa maji, kisha kuanguka na kubamiza kichwa chake Desemba 9.
Aligundulika kuwa na jeraha kwenye ubongo Desemba 13 na tangu wakati huo hakuonekana tena hadharani.

No comments: