MGOGORO WA KKKT WATINGA RASMI TUME YA USULUHISHI...

Bodi ya Udhamini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, imefikishwa mbele ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwa kumtimua kazi Mchungaji Philemon Mollel wa Usharika wa Ngateu.
Mchungaji huyo tayari amefikisha malalamiko yake CMA na kikao cha kwanza cha usuluhishi kimepangwa kufanyika Februari 5, mwaka huu jijini Arusha.
Mtoa habari wetu ndani ya Makao Makuu ya Dayosisi hiyo,  amesema tayari barua ya mwito kutoka CMA imeshapokewa na viongozi wa Dayosisi.
“Nakwambia ndugu yangu hapa sasa ni kama jehanamu, viongozi wamechanganyikiwa hakuna utulivu, kila mmoja kati ya wajumbe wa Bodi anajipanga atakavyojieleza,” alisema mtoa habari wetu.
Suala hilo limefikishwa katika Tume hiyo chini ya hati ya dharura kwa kile kilichoelezwa kuwa waumini wa Kanisa hilo wanahitaji huduma za Mchungaji huyo. 
Kwa mujibu wa Katiba ya KKKT, baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ni Askofu, Katibu Mkuu wa Dayosisi, Msaidizi wa Askofu na wajumbe wengine.
Hati hiyo ya kuitwa kwa Bodi, imeonesha kupokewa na mtumishi aliyejitambulisha kwa jina la Nicholas Mollel Januari 21, mwaka huu na wajumbe hao wametakiwa kufika mbele ya Tume wao binafsi,  au wakili wao.
“Suala hili ni la dharura na kwa kuwa wafuasi wa Kanisa langu wanahitaji utumishi wangu, ninawajibika kuwatumikia,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo ikimnukuu Mchungaji Mollel katika malalamiko hayo.
Katika taarifa hiyo, Mchungaji Mollel anailalamikia Bodi hiyo kwa kumfukuza kazi bila kumsikiliza, kinyume cha Katiba ya Kanisa hilo na kwamba taratibu zote hazikufuatwa.
Pamoja na kufukuzwa kazi bila kupewa fursa ya kujitetea, pia amedai kwamba madai yanayoelekezwa kwake kwamba alifanya makosa yasiyovumilika katika Kanisa hilo, hayakuthibitika mahali popote.
Kwa hali ilivyo, kuna kila dalili ya suala hilo kufika mahakamani kutokana na misimamo mikali ya pande hizo mbili zinazosuguana kati ya uongozi wa Dayosisi ya Kaskazini Kati kwa upande mmoja na Mchungaji Mollel.
Uongozi wa Dayosisi ulimtaka Mchungaji Mollel kuomba radhi kwa makosa anayodaiwa kufanya, yaliyosababisha afukuzwe kazi, ili asamehewe na kurudishwa kundini.
Hata hivyo Mchungaji Mollel aliwahi kusema: “Sifikirii na kamwe sitaomba radhi kwa sababu sijafanya kosa lolote kwani nilizungumza katika vikao halali vya Kanisa na sio nje ya vikao juu ya ufisadi uliokithiri ndani ya Dayosisi.
“Niliomba wahusika wachukuliwe hatua akiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya Arusha Corridor Springs Israel Ole Karyongi kujiuzulu,” alisema.
Mchungaji Mollel alifukuzwa kazi katika Kanisa hilo kuanzia Desemba 24, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni makosa yasiyovumilika ndani ya Kanisa.
Kabla ya kufukuzwa kazi Mchungaji huyo, kuliibuka mgogoro katika Kanisa hilo baada ya moja ya benki za biashara kuipa Dayosisi hiyo muda hadi Desemba 31 mwaka jana iwe imelipa deni la Sh bilioni 11, vinginevyo mali zake zingepigwa mnada.
Kutokana na taarifa hiyo ya benki, Kanisa lilitoa waraka wa Askofu ambapo waumini zaidi ya 600,000 walitakiwa kila mmoja achangie Sh 20,000 ili kunusuru mali za Kanisa zilizo hatarini kufilisiwa baada ya Hoteli ya Corridor Springs, mali ya Kanisa hilo kudaiwa fedha hizo.
Baada ya waraka huo, baadhi ya waumini akiwamo Mollel wakitaka waliohusika na uzembe uliosababisha deni hilo, wawajibike kabla ya waumini kutoa mchango huo.
Kutokana na msimamo huo, Mollel alitakiwa kuomba radhi na alipokataa, alisimamishwa kazi na kuvuliwa madaraka ya kuhudumia Usharika wa Ngateu aliokuwa akihudumia.

No comments: