WAUMINI KKKT WAAPA KUMTETEA MCHUNGAJI ALIYETIMULIWA...

Askofu Thomas Laizer.
Waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, wamekuja juu na kuahidi kuandamana kupinga hatua ya kanisa hilo kumvua cheo na kumfukuza Mchungaji Philemon Mollel aliyekuwa Kiongozi wa Usharika wa Ngateu katika Jimbo la Arusha Magharibi.
Hatua ya waumini hao imekuja baada ya Mchungaji Mollel kutuhumiwa kushupalia suala la Kanisa hilo kuchangisha waumini wake fedha ili kulipa deni linalodaiwa na benki katika kuiokoa Hoteli ya Corridor Springs, mali ya KKKT Dayosisi ya Kati, inayoongozwa na Askofu Thomas Laizer.
Katika mazungumzo kwa simu na kwa ujumbe mfupi wa maneno waliotuma baada ya kuandikwa taarifa kuhusu mgogoro ndani ya Dayosisi hiyo, waumini hao wameapa kwamba hawatakubali Mchungaji Mollel afanywe mbuzi wa kafara.
“Mimi ni Msharika wa kawaida kabisa, muumini wa kawaida kabisa wa KKKT, nashukuru sana kwa taarifa yenu ya leo (juzi). Ni kweli mliyoandika, Mchungaji Mollel amesimamishwa na sisi hatumuoni hapa kwa sababu tumeletewa Mwinjilisti, tunashangaa Mchungaji wetu yuko wapi,” alisema muumini wa usharika huo anayeishi katika Mtaa wa Kiranyi.
Muumini huyo ambaye jina tunalo, alisema hatua hiyo imewashangaza kwa sababu Mchungaji Mollel amekuwa mkweli, kwa kuwaeleza kuhusu waraka wa kuchangia kuokoa hoteli hiyo ya KKKT, lakini jambo linalowashangaza wao (waumini) ni jinsi gani faida ya hoteli hiyo inavyotumika.
“Sisi tuliyajua haya, kwa sababu Mchungaji alitueleza akijua madhara ya kutueleza jambo hili, hawataki ukweli hawa. Sasa inakuwaje sisi tuchangishwe ili kulipia hasara, faida ya hoteli ilikwenda wapi? Tunataka maelezo ya kina, kuna matatizo KKKT, na lazima yaanikwe ili kulisaidia Kanisa,” aliongeza muumini huyo.
Alisema kutokana na hatua iliyochukuliwa dhidi ya Mchungaji wao, hawatakubali kwa sababu wanaona ametolewa kafara kwa kuwa mkweli na wataandamana kuhakikisha anarejeshwa madarakani.
“Huyu Mchungaji wetu ni mtu mkweli na mchapakazi. Amekuja hapa ametusaidia sasa tumejenga Kanisa letu na liko katika hatua ya kuweka tiles (marumaru). Na sisi tulifikiri faida ya hoteli ingetumika kutusaidia sisi tuliojenga Kanisa tulikamilishe, lakini tunashangaa tunatakiwa kulipia hasara.
“Kwa kweli hatutakubali kwa sababu kuna matatizo katika kanisa letu, hata shule tunajenga, lakini sisi watu wa kawaida, hatupeleki watoto wetu kwa sababu gharama ni kubwa. Sisi tunajenga kwa faida ya nani? Ndio maana wanaosema ukweli wanafukuzwa ili kuficha matatizo,” aliongeza muumini huyo.
Habari tulizozipata baadaye jana, zilieleza kuwa waumini wanaotoka katika Dayosisi hiyo ya Kaskazini Kati, katika Jimbo la Arusha Magharibi walikutana katika hoteli moja ya jijini Arusha (jina tunalo) jana jioni kupanga maandamano ya kupinga kufukuzwa kwa Mchungaji Mollel.
Wakati muumini huyo akisema hayo, waumini wengine waliotuma ujumbe mfupi wa maneno katika simu (sms) walidai kuwa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati, imegubikwa na ufisadi na uonevu.
“Tunashukuru mnavyofuatilia hizo habari na kutupasha. Mimi niko ndani ya dayosisi hii. Mwenye msimamo ni Mchungaji Mollel. Hatua aliyochukuliwa ni kuwanyamazisha wengine kwenye hili jambo. Misaada inayotoka nje ya wafadhili ni mingi, wanaitumia huko mijini wanakotoka na haina udhibiti wala ukaguzi,” alidai muumini mwingine.
Mwingine alisema kufukuzwa kazi kwa Mchungaji Mollel siyo jambo zuri, “ila moto kwa Wakristo utawaka na bila Kanisa kuingilia kati, litashindwa kuuzuia.”
Mgogoro ndani ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati umeibuka baada ya waumini wake kupewa waraka wa kutakiwa kila mmoja kuchangia Sh 20,000 ili  kunusuru mali za kanisa zilizo hatarini kufilisiwa baada ya Hoteli ya Corridor Springs kudaiwa Sh bilioni 11 na benki moja nchini.
Hatua hiyo imepingwa na waumini hao na baadhi ya wachungaji akiwemo Mollel anayetaka wahusika wa kadhia hiyo wachukuliwe hatua; lakini akageuziwa kibao yeye na kufukuzwa na kuvuliwa madaraka ya kutoa huduma za kichungaji katika kanisa hilo nchini.
Vyanzo vyetu vya habari ndani ya kanisa hilo vilieleza kuwa hatua hiyo imetokana na Mchungaji Mollel kushindwa kutekeleza mambo matatu aliyotakiwa na Tume maalumu ya watu watatu walioteuliwa na Menejimenti ya Dayosisi hiyo na alipewa siku tatu kuomba radhi, lakini hakufanya hivyo.
Habari zilieleza kuwa walioteuliwa Desemba 14, mwaka huu na kwenda kumwona Mchungaji Mollel kutekeleza hayo ni pamoja na Msaidizi wa Askofu Mchungaji Solomoni Massangwa, Katibu Mkuu wa Jimbo Arusha Magharibi, Mchungaji Godwini Lekashu na Katibu Mkuu wa Dayosisi, Israel ole Karyongi.

No comments: