MWANAMKE ABAKWA KISHA KUCHINJWA MKOANI KATAVI...

Eneo la Ziwa Rukwa.
Mwanamke mfanyabiashara ya samaki ambaye ni mkazi wa Kyela mkoani Mbeya, Neema Mwambinga (44), amebakwa kisha kuuawa kikatili kwa kuchinjwa na watu wasiofahamika katika kambi ya uvuvi  iliyopo Mto Yeye, katika Bonde la Ziwa Rukwa, Tarafa ya Mamba wilayani Mlele, mkoani Katavi.
Akizungumza kwa simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kadavashari,  alisema mauaji hayo yalitokea Desemba 21, mwaka huu saa tano usiku katika kambi ya uvuvi, kando ya Mto Yeye katika Bonde la Ziwa Rukwa.
Akisimulia mkasa huu aliouita wa kinyama, Kamanda Kadavashari alisema mama huyo alifika kambini hapo  kununua samaki ili aende kuwauza Kyela katika msimu huu wa Krismasi na Mwaka Mpya.
Kwa mujibu wa Kamanda, usiku huo wa tukio, ‘genge’ la watu wasiofahamika walivunja nyumba alimofikia  akiwa amelala  peke yake, kisha wakambaka  kwa zamu,  na ‘wabakaji’ hao  ghafla wakambadilikia na kuanza  kumpiga  sehemu mbalimbali  za mwili  wake kisha wakamchinja  na kutokomea kusikojulikana.
Alisema taarifa za awali zinaeleza kuwa hakukuwa na uporaji wa fedha uliofanyika katika tukio hilo, lakini mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa na jeraha kubwa katika paja lake la mguu wa kushoto.
Alisema chanzo hakijafahamika “ila inawezekana ni mambo haya ya ushirikina, kwani kambi hiyo ni ya wavuvi na marehemu huyo alifika hapo kibiashara, lakini pia inawezekana walidhamiria kumbaka kisha kumtoa uhai kwani mpaka sasa hatuna taarifa ya marehemu kuporwa mali yoyote zikiwemo fedha.”
Kwa mujibu wa Kamanda, tayari watu watano wamekamatwa wakihusishwa na mauaji ya mama huyo. Alisema majina kamili ya waliokamatwa hakuwa nayo wakati huo.
Katika mkasa mwingine, Polisi mkoani Katavi kwa kushirikiana na askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) wamewakamata watu wawili wakimiliki silaha aina ya SMG isivyo halali.
Kamanda Kavadashari aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Emmanuel Kulowa (20) mkazi wa kijiji cha Kamsisi katika Tarafa ya Inyonga wilayani Mlele na Hamis Mrisho (37), mkazi wa kitongoji cha Makanyagio  mjini Mpanda wakijiandaa kusafiri, lakini kwa taarifa za siri za raia wema walikamatwa juzi saa 11 jioni.
Alisema walikamatwa na SMG yenye namba 1973221544 ikiwa na magazini mbili na risasi 25 zilizokuwa  zimehifadhiwa kwenye begi la kusafiria na kwamba wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara tu upelelezi wa awali wa shauri lao utakapokamilika.

No comments: