CHUO KIKUU MLIMANI CHA SITA KWA UBORA AFRIKA...

Sehemu ya Chuo Kikuu Dar es Salaam eneo la ukumbi wa Nkrumah.
Wakati wanafunzi wengi wa Bara la Afrika wakihangaikia kusaka elimu bora katika nchi za Ulaya na Marekani, utafiti umeonesha kuwa Afrika ina vyuo bora, huku Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kikitajwa kushika nafasi ya sita.
Kwa mujibu wa utafiti huo wa Africa.com na ambao matokeo yake yalitolewa Novemba 9, vyuo vikuu vitatu vya Misri, ndivyo vilivyoshika nafasi tatu za juu kwa ubora miongoni mwa vyuo vikuu 10 bora Afrika.
Hata hivyo, watafiti wamefafanua kuwa utafiti huo haujahusisha vyuo vya Afrika Kusini kutokana na ukweli kuwa, vina ubora wa hali ya juu zaidi, hivyo huenda vingechukua idadi kubwa katika Kumi Bora.
Ukiondoa vyuo vya Afrika Kusini, Chuo Kikuu cha Cairo kilichoanzishwa mwaka 1908, sasa kikiwa na wanachuo 45,000 wanaovuna ujuzi katika taaluma za Sayansi, Dawa, Teknolojia ya Habari na Sayansi za Siasa, ndicho kinachoshika nafasi ya kwanza Afrika. Kina zaidi ya wanafunzi 4,000 kutoka nje ya Misri.
Kinafuatiwa na Chuo Kikuu cha Marekani kilichopo Misri, kilichoanzishwa mwaka 1919. Miongoni mwa wasomi waliopikwa hapo ni pamoja na Waziri wa zamani wa Ulinzi wa Japan, Yuriko Koike.
Nafasi ya tatu inashikwa na Chuo Kikuu cha Mansoura, kilichoanzishwa mwaka 1972, lakini kikiwa na wanafunzi 100,000 waliopo katika vitivo 17 vya chuo hicho maarufu kwa masomo ya udaktari.
Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda kilichoanzishwa mwaka 1922, wakati huo kikiwa Chuo cha Ufundi kabla ya kuwa Chuo Kikuu kamili mwaka 1970, kinashika nafasi ya nne Afrika na ndicho cha kwanza kwa ubora Afrika Mashariki.
Kina idadi kubwa ya fani zinazofundishwa, huku kikiwa na wanafunzi zaidi ya 35,000 wa shahada ya kwanza pekee. Kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi, wakati wa sherehe za miaka 90 ya chuo hicho, kilizindua ujenzi wa maktaba mpya itakayokuwa kwenye eneo la meta za mraba 8,000.
Miongoni mwa wasomi wake maarufu ni pamoja na Rais wa Kwanza wa Tanzania, hayati Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Kenya, Mwai Kibaki, Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa na Askofu John Tucker Mugabi Sentamu.
Utafiti huo umekiweka katika nafasi ya tano Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya chenye wanafunzi 50,000 wa shahada ya kwanza pekee, wengi wakiwa katika vitivo maarufu kwa utafiti wa Sayansi. Mshindi wa Tuzo za Nobel, Profesa Wangari Maathai ni miongoni mwa wasomi wake wanaoheshimika, ingawa kwa sasa ni marehemu.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kilichoanza kujitegemea mwaka 1970 baada ya kuwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki, kinashika nafasi ya sita Afrika kutokana na kujikita katika utafiti mbalimbali, kikiwa pia imara katika vitivo vya Uhandisi, Sheria, Biashara na Teknolojia.
Ubora wake unaweza kupimwa kwa kutoa wasomi na viongozi mahiri wakiwamo Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni na  Dk Asha-Rose Migiro, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliyemaliza muda wake.
Kwa sasa, kikiwa na vyuo vikuu vishiriki viwili, Chuo Kikuu cha Elimu Mkwawa (MUCE) na kile cha Dar es Salaam (DUCE), asilimia tisa ya wanafunzi wake wanatoka nje ya Tanzania.
Akizungumzia utafiti huo, Msemaji wa chuo hicho, Jackson Isdory alisema chuo chuo kilichopo katika eneo la ukubwa wa ekari 1,625, Magharibi mwa Dar es Salaam, umbali wa kilometa 13 kutoka katikati ya Jiji, Msemaji wa chuo hicho, Jackson Isdory alisema chuo chake hakiwezi kuzungumzia utafiti huo kwa kuwa hawajauona.
Isdory alizungumza baada ya Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Rwekaza Mukandala kutopatikana ikielezwa yuko nje ya nchi kikazi, wakati Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taalamu, Profesa Makenya Maboko naye hakupatikana kwa simu, licha ya kuelezwa yuko nchini.
Nafasi ya saba inashikwa na Chuo Kikuu cha Botswana, kilichoanzishwa mwaka 1982. Kina idadi ya wanafunzi takribani 16, 000 hao ni wa shahada ya kwanza pekee. Chuo Kikuu cha Ghana ambacho Mkuu wake wa Chuo ni Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, ndicho kinachoshika nafasi ya nane, kikifuatiwa na Chuo Kikuu cha Lagos, Nigeria.
Chuo Kikuu cha Ashesi kilichoanzishwa miaka 10 tu iliyopita, ndicho kinachoshika nafasi ya 10 kwa ubora. Kimejikita katika Sayansi ya Kompyuta, Utawala wa Biashara na Teknolojia ya Habari. Kina baraka za Rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter na Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Benki ya Dunia, Peter Woicke.

No comments: