BERENIK AZOA MILIONI 20 ZA MAISHA PLUS 03...

Mshiriki Berenik Kimilo kutoka Dar es Salaam, usiku wa kuamkia leo ameibuka kidedea katika Shindano la Maisha Plus 03 na kufanikiwa kujinyakulia kitita cha Shilingi milioni 20.
Berenik, mama wa mtoto mmoja, Kelvin, amefanikiwa kuwabwaga 'wanaume wa shoka', Vincent Mushi aliyejinyakulia Shilingi milioni 6 kwa kushika nafasi ya pili na Justine Bayo aliyeshika nafasi ya tatu na kuweka kibindoni Shilingi milioni 4.
Tofauti na misimu miwili iliyopita, Shindano la mwaka huu ambalo safari yake ilianza Oktoba 2, lilinogeshwa na uwepo wa mgeni rasmi Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu ambaye alijazia Shilingi milioni 10 katika zawadi za washindi wawili.
Kama haitoshi, Nyalandu katika kuonesha kunogewa na kuikubali Maisha Plus aliongeza zawadi nyingine ya Shilingi milioni 7.7 kwa washiriki wengine wote waliobaki ambapo watapata kifuta jasho cha Shilingi 500,000 kila mmoja.
Waziri Nyalandu ameahidi kukabidhi kifuta jasho hicho cha fedha taslimu leo mchana kwenye Hoteli ya Serena, Dar es Salaam ambako amewaandalia washiriki wote chakula cha mchana ili kuweza kubadilishana nao mawazo.
Katika hali isiyotarajiwa mara baada ya kutoa hotuba fupi ya kushukuru, Berenik alianguka na kupoteza fahamu jukwaani kwa kile kinachodhaniwa kuwa ni kutoamini kilichotokea. Aliondolewa jukwaani na kupatiwa huduma ya kwanza pembeni.
Shindano hilo la mwaka huu lilihudhuriwa na watu maarufu kadhaa akiwamo msanii Nassib Abdul 'Diamond', Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi, Waziri wa zamani wa Utalii na Maliasili, Shamsa Mwangunga, Balozi wa Burundi na wengineo wengi.
Pia kwa mara ya kwanza, Maisha Plus mwaka huu ilishirikisha washiriki wawili kutoka nchini Burundi, Nelly na Hatungimana Athumani.

No comments: