WAZIRI AZIFUTIA LESENI KAMPUNI ZA UAGIZAJI MAFUTA, BODI YA MAFUTA

Waziri Profesa Sospeter Muhongo.

Kufuatia kuzorota kwa upatikanaji wa bidhaa ya petroli nchini, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ametangaza kufuta leseni kwa kampuni zilizopewa kibali cha kuagiza mafuta, baada ya kubaini haziagizi bidhaa hiyo hivyo kuisababishia Serikali hasara kubwa.
Waziri pia amevunja bodi ya Kampuni iliyokuwa ikiratibu Uagizaji wa Mafuta (PIC) baada ya kubaini kuwa wajumbe wote walikuwa ni wafanyabiashara wasiokomaa kibiashara. 
Alitangaza uamuzi huo jana mbele ya waandishi wa habari katika kikao ambacho pia wafanyabiashara wa mafuta walialikwa ili kupewa uamuzi huo wa Serikali.
Uamuzi huo unatokana na maeneo mengi nchini kukosa huduma za mafuta, hali iliyosababisha usumbufu mkubwa hasa mikoani na baadhi ya maeneo katika Jiji la Dar es Salaam na hivyo kufanya wananchi wengi kuilaumu Serikali kutokana na uhaba wa bidhaa hiyo muhimu katika uchumi wa nchi.
“Kwanza kabla ya sijatoa tamko rasmi, naomba nitangulie kuwaomba radhi Watanzania kwa usumbufu waliopata wa ukosefu wa mafuta, kitendo kilichosababisha hata vyakula kupanda bei madukani pamoja na nauli,” alisema Profesa Muhongo.
Aliongeza kusema kuwa radhi hiyo anaiomba baada ya kubaini kwamba kuna uzembe umefanyika kwa makusudi huku kukiwa na mafuta ya kutosha.
Aliongeza kuwa sababu nyingine iliyosabisha kuwapo na tatizo hili ni mvutano wa kizembe uliokuwapo kati ya Mamlaka Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Bodi ya PIC pamoja na wafanyabiashara.
“Kutokana na mvutano huo baadhi ya wafanyabiashara waliamua kupeleka mafuta nje ya nchi na wengine kutunza kwenye maghala yao bila sababu ya msingi huku wakisingizia bei elekezi iliyotolewa na Ewura haiwapi faida,” alisema waziri huyo.
Kutokana na hali hiyo, ndipo Profesa Muhongo alisema muda umefika mwisho wa kuoneana aibu kwa wale wanaoshindwa kutimiza majukumu yao kulingana na leseni zao zinavyowaelekeza.
Alisema kuna baadhi ya kampuni zilipewa leseni ya kuagiza mafuta, lakini biashara zao zilikuwa za mfukoni na kuisababishia Serikali hasara na usumbufu, kampuni hizo ndani ya miezi sita hazikuleta mafuta nchini. 
Kwa hali hiyo, Waziri Muhongo alisema, “hivyo naiagiza Ewura kuzifutia leseni kampuni hizo haraka na wampelekee taarifa siku ya Jumatatu mchana na hatua zaidi zichukuliwe.
Kuhusu Bodi ya PIC inayoongozwa na Mbunge wa Kwimba, Shaniff Mansour, Profesa Mulongo alisema ameifumua na kwamba ataisuka upya na amefanya hivyo baada ya kubaini bodi yote ilikuwa ya wafanyabiashara na kazi kubwa iliyokuwa ikifanyika ni kulinda biashara yao.
“Sasa Bodi mpya itayoundwa itakuwa ya kisasa na itakuwa na mjumbe mmoja mmoja kutoka idara husika na mwenyekiti atatoka wizarani,” alisema Profesa Muhongo.
Wajumbe wengine watatoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari
Tanzania (TPA) na Kampuni ya Kimataifa ya Kuhudumia Makontena Tanzania (TICTS), PIC, na Ewura.
Profesa Muhongo alisema Bodi hiyo itaanza kazi Jumanne ijayo na endapo tatizo litajirudia, kama ni upande wa Serikali itawajibika na watendaji watafukuzwa kazi na kama ni upande mwingine utawajibishwa na Serikali.
“Taifa haliwezi kupata msukosuko kwa sababu ya watu wachache, kama kuna mtu anaona kasi hii hawezi kwenda nayo kwa kutimiza majukumu aseme wazi,” alisema Profesa Muhongo.
Hatua hiyo imekuja baada ya Katibu Mkuu wa wizara yake, Eliakim Maswi kuitaka Ewura kuhakikisha inapeleka mafuta mikoani agizo ambalo bado halijapunguza kero ya bidhaa hiyo.
Katikati ya wiki, PIC iliihakikishia Serikali kuwa kuna mafuta ya kutosha na upungufu huo umetokana na kampuni mama kukataa kuuza mafuta yao kwa vituo ambavyo havina kampuni zinazoagiza mafuta nje ya nchi.
Katika kujitahidi kupunguza uhaba wa mafuta uliopo nchini, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imesema imekubaliana kupunguza asilimia 50 ya mafuta yaliyokuwa yasafirishwe kwenda nje ya nchi na kuamua yatumike nchini. 
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Meneja wa Mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo alisema wamefikia uamuzi huo ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa mafuta uliopo kwa sasa. 
Kaguo alisema kiwango cha mafuta yaliyopo kwa sasa kwa dizeli kuna lita zaidi ya milioni 38 ambayo yatatosha kwa muda wa siku 10, petroli zaidi ya milioni 16 kwa siku tisa, jet 1 lita milioni 11 kwa siku 25 na mafuta ya taa lita 558,180 kwa siku tatu. 
Aidha, alisema kuna meli zinazotarajiwa kuingia nchini kati ya Novemba 7 mpaka 9, kwa ajili ya kuleta mafuta ambayo ni zaidi ya lita milioni 50 hivyo kupunguza tatizo hilo. 

No comments: