MHARIRI KAMPUNI YA BUSINESS TIMES APIGWA RISASI NA MAJAMBAZI...


Mnaku Mbani Lukanga akiwa amelala kitandani katika Hospitali ya Muhimbili.
Habari zilizotufikia hivi punde zinasema kwamba Mnaku Mbani Lukanga, Mhariri wa magazeti yanayomilikiwa na kampuni ya Business Times amepigwa risasi usiku huu na watu wanaoshukiwa kuwa ni majambazi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Mnaku amekimbizwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam kwa matibabu kufuatia majeraha ya risasi aliyopata katika tukio hilo.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, inasemekana kuwa alivamiwa na watu asiowafahamu akiwa njiani kuelekea nyumbani kwake Mbagala akitokea ofizi za magazeti hayo zilizoko katika Mtaa wa Lugoda, Gerezani na kumnyang'anya funguo za gari lake.
Baada ya kumnyang'anya funguo, mtu mwingine aliyekuwa na bunduki akafyatua risasi iliyopiga mdomoni na kutokea shavuni ambapo meno matatu yameng'oka.
Haikuweza kufahamika mara moja endapo kuna upotevu wa vitu wala thamani ya uharibifu wa mali zozote za Mnaku.
Tunaendelea kufuatilia taarifa zaidi kuhusu tukio hilo kwa Kamanda wa polisi kuweza kupata taarifa zaidi.

No comments: