BINTI WA MIAKA 15 AFARIKI WAKATI AKITOLEWA MIMBA MWANZA...

Sehemu ya Jiji la Mwanza.
Polisi mkoani Mwanza inamshikilia Mganga wa Zahanati ya Kiloleli katika Kata ya Nyamanoro wilayani Ilemela, Dk Lameck Msafiri kwa kusababisha kifo cha mtoto wa miaka 15 wakati akimtoa mimba.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Lily Matola alisema Msafiri alisababisha kifo cha mtoto huyo juzi saa 3 usiku.
Kwa mujibu wa Kamanda Matola, mimba ya mtoto huyo ilikuwa ya miezi minne na kabla ya kufariki, alikuwa akiishi na wazazi wake katika eneo la Kilimahewa, jijini hapa.
Matola alisema Dk Msafiri anashikiliwa kwa mahojiano zaidi na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.
Wakati huo huo, wanafunzi 30 wa Shule ya Msingi Lake B pamoja na mwalimu wao wamenusurika kufa baada ya kujeruhiwa na radi kali iliyopiga juzi saa 4 asubuhi wakati wakiwa darasani.
Kamanda Matola alisema ajali hiyo ilitokea wakati wanafunzi hao wa darasa la pili wakiwa darasani pamoja na mwalimu wao. Alisema walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure kwa matibabu.
Alisema mwanafunzi Felix Revocatus (8) hali yake sio nzuri na amelazwa hospitalini hapo huku wengine wakitibiwa na kuruhusiwa.
Katika tukio jingine, mvua kubwa inayoendelea kunyesha jijini Mwanza imesababisha kifo cha mtoto wa miezi mitatu, Ashfat Abdsalama baaada ya mtoto huyo pamoja na wazazi wake kuangukiwa na ukuta wa nyumba wanayoishi wakati wakiwa ndani.
Akifafanua Kamanda Matola, alisema juzi saa 4 asubuhi katika eneo la Kirumba Mlimani B, Abdsalama Hussein (30) na mkewe Nardia Geresheni (25) pamoja na mtoto wao, walidondokewa na ukuta wa nyumba baada ya ukuta huo kudondokewa na jiwe.
Alisema majeruhi hao walipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu, lakini baadaye mtoto huyo alifariki dunia na hali za baba na mama pia sio nzuri.

No comments: