ZUNGU ASHINDA UCHAGUZI CCM LICHA YA MADAI YA RUSHWA...

Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu.
Pamoja na kukamatwa kwa tuhuma za kudaiwa kukutwa akitoa rushwa ili kupata uongozi, Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu ameibuka kidedea katika nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia Jumuiya ya Wazazi.
Jumanne wiki hii, Zungu alikamatwa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) akiwa na wapambe wake watatu akidaiwa kutoa rushwa kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi, ili wamchague awe Mjumbe wa NEC.
Hata hivyo, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Eunice Mmari alimwachia Mbunge huyo wa Ilala na Mwenyekiti wa Bunge, kwa dhamana na kuongeza kuwa uchunguzi wa tuhuma hizo unaendelea na ukikamilika, atafikishwa mahakamani.
Saa chache baada ya kuachiwa kwa dhamana hiyo, Zungu alikuwa ndani ya ukumbi wa uchaguzi ambako aliibuka kidedea NEC kwa kupata kura 402, akiwa nyuma ya Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima aliyepata kura 531 na Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza aliyepata kura 448.
Miongoni mwa walioshindwa ni Said Bwanamdogo, Dk Salim Chikago, Menrad Kigola, Paulo Kirigini, Murtaza Mangungu, Stella Manyanya, Vita Kawawa, Pricilla Mbwaga, Clementina Mollel, Bernard Murunya, Thobias Mwilapwa, Esther Nyawazwa, Dk Charles Tizeba na Jeremia Wambura.
Kwa nafasi hiyo ya ujumbe wa NEC Zanzibar nafasi mbili walioshinda ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima aliyepata kura 479 na Fatma Abeid Haji alipata kura 415.
Nafasi ya ujumbe wa Baraza Kuu Tanzania Bara walioshinda ni Dk Godbertha Kinyondo, Saumu Mohamed Bendera, Deogratias Rutta, Masudi Bwire na Juliana Chintika; wakati kwa Zanzibar ni Yasmini Yusfal Alloo (229),  Khamis Suleiman Dadi (221), Bakari Hamad Khamis (332),  Ali Haji Ali (192) na Haji Mwita (192).
Nafasi ya uwakilishi wa Mkutano Mkuu katika Jumuiya ya Wanawake aliyeshinda ni Godlever Kamala na uwakilishi katika Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Vijana (UVCCM) ni William Malecela aliyepata kura 574 na kuwashinda Talib Ali Talib aliyepata kura 217 na Namelok Sokoine aliyepata kura 107.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo usiku wa kuamkia jana, Msimamizi Mkuu wa uchaguzi huo, Steven Wasira alisema Abdalah Bulembo alishinda nafasi ya Mwenyekiti kwa kupata kura 677 na kuwaacha Martha Mlata aliyepata kura 192 huku John Barongo akiambulia kura 42.
Nafasi ya Makamu Mwenyekiti ilikwenda kwa Dogo Idd Mabrouk aliyetetea kiti chake baada ya kupata kura 417 na kuwashinda wagombea wenzake Ally Issa Ally na Hassan Rajab Hatibu.
Wakati tuhuma za Zungu zikichunguzwa, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete amesema dawa ya wala rushwa ndani ya chama hicho kwa sasa inatafutwa ili kukomesha tabia ya kuuza na kununua kura.
Akifunga mkutano huo jana, Rais Kikwete alisema lazima awaambie ukweli kuwa chama kinatukanwa kwa sababu ya watu wanaoendekeza tabia ya kununua na kuuza kura.
“Wanaofanya hivyo wanajijua na wengine wako humu humu ndani, lakini dawa ya wala rushwa ndani ya chama inatafutwa,” alisema Rais Kikwete huku akishangiliwa na wajumbe.
Aliwataka kujua jema na baya na sura inayojengeka sasa si nzuri sana kwani vitendo vya rushwa vimekichafua sana chama na sasa jitihada zinafanyika ili kuhakikisha rushwa inadhibitiwa katika chama.
Pia Rais Kikwete alimpongeza Mwenyekiti mpya Bulembo kwa kuchaguliwa kushika wadhifa huo na Dogo Idd Mabrouk kwa kuchaguliwa tena kuwa Makamu Mwenyekiti.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo alisema tathimini iliyofanyika tangu 1995 inaonesha kuwa jumuiya hiyo haijaonesha kama ilichangia ushindi wa CCM katika Uchaguzi Mkuu.
“Kati ya jumuiya tatu; wanawake na Vijana wanaongoza, Wazazi hapana, ukweli ndiyo huo, kaeni chini mjiulize, cha muhimu ni kujiuliza mtakuwaje tofauti na kuona mtafanya nini …lakini lazima mjue ukweli, wazazi sio sana nisipowaambiwa mimi  hakuna wa kuwaambia,” alisema.
Wagombea wa nafasi ya uenyekiti walioshindwa Barongo na Mlata juzi usiku walisusa kusaini karatasi ya matokeo.
Wakati mshindi wa nafasi hiyo, Bulembo alipopewa nafasi ya kujieleza alisema anasikitishwa na kitendo cha wenzie kugoma kuweka saini kwenye matokeo hayo.
Mwenyekiti wa muda wa mkutano huo, Mary Chatanda alipowaita wagombea hao kwenye saa tano usiku ili kuzungumza maneno machache, wagombea wote hawakutokea kwa kuwa walishaondoka ukumbini.

No comments: