WASICHANA 25,000 KWA SIKU KUOLEWA WAKIWA CHINI YA MIAKA 18...

Wasichana hawa wadogo nchini Afghanistan wakiwa na waume zao ambao ni rika sawa na baba au babu zao.
Akiwa na umri wa miaka 11, Ghulam aliolewa na Jaiz mwenye miaka 40 katika eneo la kijijini nchini Afghanistan, na kumfanya kuwa mmoja kati ya wasichana wadogo zaidi ya milioni 10 ambao wamekuwa wakilazimishwa kuolewa na wanaume wazee kutosha kuitwa baba au babu zao kila mwaka.
Katika juhudi za kuanzisha mjadala wa kimataifa kuhusu madhara ya ndoa za mapema, ambazo kwa sasa zimekuwa zikiendelea katika zaidi ya nchi zinazoendelea 50, Umoja wa Mataifa umeitangaza Oktoba 11 kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Watoto wa Kike mwaka huu.
Katika kuadhimisha siku hiyo na kuweka mkazo kwenye tatizo la ndoa za watoto, mpigapicha Stephanie Sinclair aliungana na National Geographic kuandaa mfululizo wa picha za kutia uchungu zikionesha wasichana wadogo wa hadi miaka mitano wakiolewa na wanaume wa rika la kati katika nchi kama India, Yemen na Ethiopia.
Ingawa ndoa za watoto ni kinyume cha sheria katika nchi nyingi, na mikataba ya kimataifa inapinga vitendo hivyo, inakadiriwa kwamba zaidi ya wasichana milioni 51 walio chini ya miaka 18 kwa sasa wameolewa, wachache ikiwa gizani na kwa siri kubwa. Afghanistan pekee, inaaminika kwamba takribani asilimia 57 ya wasichana wameolewa kabla ya umri wa miaka 16 unaoruhusiwa kisheria.
Mambo mbalimbali yanashawishi wazazi wa wanandoa watoto kuwaozesha wasichana wao, kuondokana na shinikizo la jamii kuthibitisha mila za kitamaduni zilizopitwa na wakati kukabiliana na hali ya kiuchumi. Katika mataifa maskini, yanayoendelea, si jambo la ajabu kwa familia kulipia madeni yao kwa kuwatoa mabinti zao kama malipo.
Mbali na India, ambako wasichana kwa kawaida wanaolewa na wavulana ambao huishi pamoja pale tu wanapokuwa wakubwa, waume wanaweza kuwa wakubwa kwa miaka muongo mzima kuliko wake zao watarajiwa. Si jambo la kushangaza kwa wanaume kuwateka njara wasichana na kuwabaka kwanza kabla ya kujaribu kufunga ndoa.
Tangu mwaka 2003, Stephanie amekuwa akisafiri kwenye kona za dunia zisizofikika kirahisi katika nchi kama Nepal na Yemen kuandika ndoa za maharusi watoto na safari yao kuelekea kuwa mama vijana katika matarajio ya kuwapatia sauti na kuibua utayari wa tatizo hilo.
Wataalamu wamekubali kwamba ndoa za mapema zinawakwamisha wasichana kupata elimu na kuwapora haki yao ya utoto sababu wake wengi vijana, wamekuwa wakibeba zigo la majukumu ya kikubwa, hawapati nafasi ya kujichanganya na wenzao wa rika moja au kuunda urafiki nje ya ndoa zao.
Ghulam, mwanandoa mwenye miaka 11 kutoka Afghanistan ambaye ameolewa mwaka 2005, alilazimishwa kuacha shule na kukatisha ndoto zake za kuwa mwalimu siku moja. Wazazi wamekuwa wakiwaondoa binti zao shuleni hata kabla ya kuchumbiwa ili kudhibiti kujichanganya na wavulana.
Katika matukio mengi, wasichana hao wamekuwa wakitawaliwa na waume zao na mashemeji, na kuwaingiza kwenye ugomvi mkubwa wa kifamilia na pia mateso ya kimwili, kingono na matusi.
Wake wenye umri mdogo ambao wamebahatika kuwatoroka waume zao huishia kuishi katika umaskini, au maisha magumu. Baadhi ya wasichana wamejiingiza kwenye umalaya kujipatia kiasi kidogo cha kujikimu kimaisha na kuingia katika madanguro, ambako wamekuwa wakijikuta katika udhalilishaji wa kutisha zaidi.
Wengi wa wasichana hao ambao huingia katika ndoa za mapema wanatarajiwa kupata ujauzito mara moja, hali ambayo mara kadhaa imekuwa ikiwaingiza kwenye janga kwa mama wote, ambao wenyewe pia bado ni watoto, na watoto zao.
Isipokuwa tu mashirika ya kimataifa yatakapochukua hatua kubadili mwenendo huu, inakadiriwa kwamba katika muongo unaokuja, wasichana zaidi ya milioni 100 - au karibu wasichana 25,000 kwa siku - wataolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.

No comments: