WANAJESHI WA JWTZ WAMSHUSHIA KIPIGO KIKALI TRAFIKI UBUNGO...

Matrafiki na Askari wa Doria wakiwa wamekusanyika katika taa za kuongozea magari eneo la Ubungo baada ya mwenzao kupigwa vibaya na wanajeshi na kukimbia jana mchana.
Jeshi la Polisi katika Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, linawashikilia askari watatu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa tuhuma za kumpiga askari polisi wa kikosi cha usalama barabarani `trafiki’   wakati akiwa kazini eneo la Ubungo Mataa, Dar es Salaam.
Tukio la kupigwa kwa askari huyo ambaye hata hivyo jina lake halikuweza kufahamika mara moja, lilitokea jana saa 4:15 asubuhi katika eneo la taa za kuongozea magari Ubungo, baada ya wanajeshi hao kumtuhumu askari huyo kuwa amewaweka muda mrefu katika foleni.
Wanajeshi hao waliokadiriwa kuwa zaidi ya saba, walikuwa ndani ya gari la jeshi wakitokea eneo la Mwenge kuelekea Buguruni.
Lakini baada ya kusota katika foleni kwa muda mrefu kama ilivyokuwa kwa magari mengine, askari hao walishuka kutoka katika gari lao mmoja baada ya mwingine na kwenda kumvamia trafiki huyo na kuanza kumpiga makofi na mateke, mashambulizi yaliyomzidi nguvu askari huyo wa kikosi cha usalama barabarani na kujikuta akianguka chini.
Licha ya trafiki huyo kuwaomba msamaha wanajeshi hao, hawakuweza kusikia kilio chake na kuendelea kumpiga katikati ya barabara hiyo huku wananchi wakishuhudia.
Hata hivyo baada ya kutimiza azma yao hiyo wanajeshi hao walimuacha askari huyo na kwenda kupanda katika gari lao na kuendelea na safari huku askari huyo akijaribu kuomba msaada kwa wenzake kwa kuwapigia simu.
Muda mfupi baadaye gari la polisi lililokuwa na askari wenye silaha lilifika katika eneo hilo na kuanza kuwafuatilia wanajeshi hao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Charles Kenyela, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa waliwakamata wanajeshi hao muda mfupi baada ya kuondoka eneo la tukio.
Bila kumtaja askari aliyepigwa wala idadi kamili ya wanajeshi wanaoshikiliwa, Kenyela alisema atazungumza rasmi kuhusu jambo hilo kesho (leo), “Tuliwakamata wanajeshi hao eneo la Buguruni, hadi ninavyokuambia wapo mikononi mwetu, tunaendelea na upelelezi ili kujua sababu za wao kufanya hivyo na kesho (leo) tutaeleza kila kitu,” alisema Kenyela.
Wakizungumzia kuhusu kitendo hicho baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo, wameshauri askari hao wa JWTZ wachukuliwe hatua kali ili iwe fundisho kwa wanajeshi wengine wenye tabia kama hizo.
Mmoja wa wananchi aliyejitambulisha kwa jina la Yahaya Kimaro, alisema kitendo kilichofanywa na wanajeshi hao ni cha udhalilishaji na kwamba hakipaswi kurudiwa.
Alisema inashangaza kuona walinzi hao wa usalama wa nchi na wananchi wake wanashindwa kuthaminiana wenyewe na kufanya unyama huo. Hili ni tukio la pili kwa askari wa usalama wa barabarani kupigwa na wanajeshi akiwa kazini kwa madai ya kuwachelewesha kwenye foleni kwani tukio la kwanza lilitokea Mei 19, 2009, kitendo ambacho kinachukuliwa kama mwingiliano wa kazi.

No comments: