DK MWAKYEMBE AHUJUMIWA BANDARINI DAR...

Sehemu ya bandari ya Dar es Salaam.

Kamati iliyoundwa na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe kuchunguza utendaji wa kazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari ya Tanzania (TPA) imefanyiwa hujuma wakati ikitekeleza uchunguzi huo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo yenye wajumbe saba, Bernard Mbakileki alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akikabidhi matokeo ya ripoti ya uchunguzi wa utendaji wa bandari hiyo kwa Waziri Mwakyembe.
Kwa mujibu wa Mbakileki moja ya vitendo vya hujuma walivyokutana navyo wakati wakitekeleza majukumu yao ni baadhi ya watu waliotakiwa kukwepa kuhojiwa.
“Mheshimiwa Waziri naomba nikukabidhi ripoti hii rasmi na kukufahamisha kuwa tumemaliza kazi uliyotupa lakini katika utendaji wetu yaliyojiri ni pamoja na baadhi ya wahojiwa kukwepa kuhojiwa wakisingizia kuumwa, kufiwa na wengine hata simu hawakupokea,” alisema Mbakileki.
Alisema kulitokea pia jaribio la wizi wa kompyuta lililofanyika katika kituo cha Wakala wa Vipimo (WMA) bandarini, ambalo kamati hiyo ililichukulia kuwa lengo lilikuwa kupoteza ushahidi.
Kutokana na jaribio hilo, Mbakileki alisema alizungumza na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Temeke na maofisa wengine wa Polisi kuhusu jaribio hilo na pia kukamatwa kwa magari yanayobeba mafuta machafu bandarini.
Baada ya kupewa taarifa hiyo, Dk Mwakyembe aliihakikishia kamati hiyo kuwa wale wote waliohujumu uchunguzi huo kwa kukwepa kuhojiwa na waliohusika katika jaribio la wizi wa kompyuta sasa watahojiwa mbele yake na iwapo kutakuwa na haja ya Polisi, watahojiwa pia polisi.
Akizungumzia utendaji wa bandari, alisema ilikuwa lazima kamati iundwe kuchunguza chanzo cha utendaji mbovu kwa kuwa hali ilikuwa mbaya hadi kusababisha bandari hiyo kuingia kwenye kumbukumbu za kimataifa kwa udokozi na kukosa ufanisi.
Aliwahakikishia Watanzania kuwa ifikapo Desemba mwaka huu, sura ya utendaji kazi wa bandari ya Dar es Salaam itabadilika kwa kuimarika na kuwa chombo namba moja kitakacholipatia taifa mapato.
“Nilidhani Tanzania tutaingia kwenye rekodi ya kuwapandisha twiga kwenye ndege pamoja na urefu wao, lakini sasa tumeingia hadi kwenye kumbukumbu za kimataifa kwa udokozi, nawahakikishia hili la udokozi litakwisha na kila aliyehusika naye lazima adokolewe,” alisema Dk Mwakyembe. 
Alisema bandari hiyo haikuwa na ufanisi katika upakuaji wa mizigo na badala ya kuchukua siku nne kama bandari nyingine, ilikuwa inapakua kwa siku 10 hadi 24.
Mbali na kupoteza muda, Dk Mwakyembe alisema pia ilikuwa na wizi wa makontena ambapo mwaka juzi makontena 10 yalitoweka, mwaka jana 26 na mwaka huu mpaka sasa mawili yameshapotea hali iliyopoteza uaminifu wa bandari hiyo ndani na nje ya nchi.
Hata hivyo, alisema kwa sasa baada ya uchunguzi kufanyika na menejimenti kupumzishwa, hali imeanza kuimarika bandarini hapo kimapato lakini pia mawaziri wa nchi nne ikiwemo Burundi, Rwanda na Congo wameshaonesha nia ya kurejea kutumia tena bandari hiyo.
Alisema pamoja na mafanikio hayo pia boya la mafuta lililipo bandarini litaanza kufanyakazi Novemba mwaka huu, hali itakayoruhusu meli za mafuta kubwa kuja moja kwa moja kupakua mafuta badala ya meli ndogo ambazo zilikuwa zikigharimu fedha nyingi na kuchangia bei ya mafuta kuwa juu.
Naye Naibu Waziri wa Uchukuzi Charles Tizeba, aliwataka watendaji wa bandari waliobaki kushiriki kikamilifu kuleta mabadiliko ya kiutendaji katika bandari hiyo badala ya kuwa kikwazo na wale wanaoona hawakubaliani na mabadiliko hayo, wakatafute kazi kwingine.
Kamati hiyo iliteuliwa Agosti 27 mwaka huu na kuanza kazi Agosti 31. Ilipewa hoja 34 za kufanyia kazi zilizo kwenye mfumo wa maswali ambazo ziliundiwa hadidu za rejea tisa.
Katika uchunguzi, kamati hiyo ilihoji watu 116 wakiwemo wajumbe wa bodi ya bandari, wafanyakazi, wawakilishi wa wafanyabiashara, maofisa wa Serikali, wastaafu wa TPA, raia wema na wageni wenye uzoefu na TPA.
Kamati hiyo pia ilipitia nyaraka mbalimbali zikiwemo sheria mbalimbali pamoja na Katiba ya nchi. Sheria zilizopitiwa ni pamoja na Sheria ya Bandari, Sheria ya Mashirika ya Umma, Sheria ya Msajili wa Hazina, Sheria ya Manunuzi na Sheria ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa. Pia ilipitia mikataba na zabuni mbalimbali za mamlaka hiyo.

No comments: