WALIOMUUA POLISI KWA KUMKATA MAPANGA ZANZIBAR WAKAMATWA...

Watu wasiofahamika wakiwa wamechoma moto barabarani katika eneo la Darajani.
Habari kutoka Zanzibar  kuhusiana na vurugu hizo zinasema  watu sita wamekamatwa kwa tuhuma za kumuua Afisa wa Polisi, Said Abdulrahman.
Taarifa ya Idara  Habari (MAELEZO) Zanzibar iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana ilisema Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa aliwaambia waandishi wa habari kwamba watuhumiwa hao (majina yanahifadhiwa) walikamatwa sehemu tofauti visiwani humo.
Kamishna huyo alisema  mmoja  wa watuhumiwa hao alikamatwa  Kisiwa kidogo cha Tumbatu, wa pili maeneo ya Mjini Unguja, mtuhumiwa wa tatu alikamatwa ofisi za Idara ya Uhamiaji alikokwenda kushughulikia hati ya kusafiria ili aweze kutoroka  nchini.
Kamishna Mussa alisema watuhumiwa wengine watatu wamekamatwa mkoani Tanga ambako walikimbilia kujificha baada ya kufanya mauaji ya Ofisa Polisi Koplo Said Abdulrahman.
 “Watu hao walitorokea huko na tunaendelea kuwahoji…tunawashukuru wananchi kwa ushirikiano wao mkubwa uliotuwezesha kufanikisha ukamataji huo, tunavishukuru vikundi vya ulinzi shirikishi vilivyo katika Shehia mbalimbali kwa kuimarisha ulinzi wa maeneo yao katika kipindi chote cha fujo na vurugu hizo,” alisema Kamishna Mussa.

No comments: