POLISI YAKAMATA WATU 53 KATIKA VURUGU ZA WAISLAMU DAR..

Kamanda Suleiman Kova.
Wakati hali ya usalama katika Jiji la Dar es Salaam imerejea kuwa shwari, Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, imesema inawashikilia watu 53 walioshiriki katika vurugu zilizotokea juzi.
Vurugu hizo zilizuka baada ya polisi kupambana na watu wanaodaiwa kuwa waumini wa dini ya kiislamu waliotaka kuandamana kuelekea Ikulu kushinikiza kuachiwa huru kwa Shekhe Ponda Issa Ponda aliyekamatwa kwa uchochezi.
Mwandishi alishuhudia mitaa mbalimbali ya Jiji ikiwa shwari huku magari kadhaa yenye polisi yakionekana yakiranda katika maeneo ya Kariakoo, Posta, Magomeni na Kinondoni, kudhibiti chokochoko zozote endapo zingejitokeza.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alithibitisha hali ya usalama kurejea katika hali ya kawaida kutokana na ulinzi kuimarishwa katika viunga mbalimbali vya Jiji.
Akizungumzia kukamatwa kwa waliohusika na vurugu za juzi, Kamanda Kova alisema hadi sasa watu 53 wanashikiliwa kwa kuhusika na vurugu hizo.
“Hali ni shwari na shughuli zinaendelea kama kawaida na tunawasihi watu wasijihusishe na vurugu kama hizo za jana kwani  zinahatarisha amani na utulivu wa nchi,” alisisitiza.
Alisema watu hao walikamatwa katika eneo la Kariakoo kutokana na kuhusika na makosa kadhaa yakiwemo ya kuwarushia mawe polisi waliokuwa katika doria.
“Vipigo ambavyo baadhi ya waandamanaji walipigwa ni vya kawaida katika hali kama ile ya vurugu ili kutuliza ghasia, lakini hakuna mtu aliyeumia kutokana na vipigo hivyo au kufikishwa hospitalini,” alisema Kamanda Kova.

No comments: