SHEKHE FARID WA UAMSHO KULA IDD EL HAJJ GEREZANI...

Wafuasi wa Uamsho wakitoka mahakamani huku wakiwa chini ya ulinzi mkali.
Mahakama ya Vuga mjini Unguja, imetupilia mbali ombi la dhamana kwa kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho, Shekhe Farid Hadi Ahmed na wenzake sita na hivyo kuwafanya kusherehekea Sikukuu ya Idd el-Hajj katika gereza kuu la Kinua Miguu mjini hapa.
Mrajisi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, George Kazzi anayesikiliza kesi hiyo  alitangaza uamuzi wa kuahirisha kesi hiyo hadi tarehe 8 mwezi ujao, kwa sababu mbili; kubwa ikiwemo hakimu aliyesikiliza kesi hiyo awali hakuwa na mamlaka ya kusililza kesi hiyo.
Aidha Mrajisi Kazzi alisema watuhumiwa wamenyimwa dhamana kwa sababu za usalama kwa kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  (SMZ).
Awali watuhumiwa hao walisomewa mashtaka matatu mbele ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Raya Mselem ikiwemo   mwaka huu kushawishi kufanya fujo na vurugu.
Aidha tarehe 26 Mei hadi Oktoba 17 huko Lumumba pamoja na Fuoni mjini hapa waliendesha mhadhara wakitoa maneno ya kashfa yenye kuhatarisha amani na usalama wa nchi.
Mwendesha mashtaka Raya alisoma shtaka la tatu ikiwa kula nyama za kujificha kwa Sheikh Farid Hadi Ahmed na kusababisha mtaharuki mkubwa kwa wananchi kulikopelekea kuzuka kwa fujo na vurugu zilizosababisha uharibifu mkubwa wa mali za wananchi kinyume na sheria kifungu 399 sheria nambari 6 ya mwaka 2004.
Mapema wakili wanaowatetea watuhumiwa na viongozi wa jumuiya ya uamsho Abdalla Juma na Salum Toufiq walilazimika kuondoka katika mahakama hiyo kwa madai kwamba wamekuwa
wakihangaishwa na kukosa mawasiliano na taarifa kamili kutoka kwa wateja wao.
Awali wananchi wengi pamoja na waandishi wa habari walifika katika mahakama ya Mwanakwerekwe ambayo awali ilisikiliza kesi hiyo, lakini kumbe watuhumiwa hao walifikishwa katika mahakama ya Vuga mjini hapa.

No comments: