DALADALA YA TRENI DAR KUANZA RASMI JUMATATU IJAYO...

Waziri wa Uchukuzi, Dk Harisson Mwakyembe amesema kuwa usafiri wa treni katika Jiji la Dar es Salaam utaanza Jumatatu wiki ijayo.
Akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Kampuni ya Reliu (TRL), Dk Mwakyembe alisema siku hiyo saa 12 asubuhi atafanya uzinduzi mdogo wa usafiri huo na baadaye watamwomba Waziri Mkuu Mizengo Pinda kufanya uzinduzi mkubwa wa mpango huo ambao umebuniwa na uongozi wa wizara hiyo.
Waziri huyo alisema kutokana na juhudi zilizofanywa na wafanyakazi wazalendo wa TRL wamefanikiwa kutengeneza na kukarabati mabehewa na injini za kampuni ambazo zilikuwa mbovu na hivyo kuwezesha usafiri huo uweze kuanza siku hiyo ya Jumatatu.
"Napenda kuwashukuru wafanyakazi kwani licha ya kutokuwepo bajeti ya mpango huu na ndani ya muda mfupi baada ya kuwaombeni kufanya kazi hii ya kukarabati mabehewa na injini mbovu, mmefanya hivyo na tarehe 29 mwezi huu tutazindua usafiri wa treni katika Jiji la Dar es Salaam," alisema Mwakyembe.
Usafiri huo unaanza baada ya kukamilika kwa ukarabati wa mabehewa 14 na injini 2 hivyo kuwezesha mpango huo ambao unalenga kupunguza kero ya usafiri katika jiji la Dar es Salaam.
Kwa kuanzia usafiri huo utakuwa kati ya Ubungo hadi Stesheni na baadaye utafuata maeneo mengine ambako kuna reli ya Kati na ile ya Tazara.
Waziri huyo pia alisema Serikali kwa kutambua umuhimu wa TRL ndio maana imetenga fedha kwa ajili ya kukarabati miundombinu za kampuni hiyo ili kuweza kuinua uchumi wa nchi.
Alisema ili kufanikisha hilo, Serikali imetenga Sh bilioni 104 kwa ajili ya kufanya ukarabati na ununuzi wa vitendea kazi na akaeleza kuwa miongoni mwa kazi zitakazofanywa kwa fedha hiyo ni ukarabati wa injini tatu, behewa 22 za abiria, mabehewa ya mizigo 125 na kununua mabehewa mengine ya mizigo 274 na behewa za breki 43.
Alisema Sh bilioni 18.9 kati ya hizo zitatumika kukarabati karakana mbalimbali za kampuni hizo zilizoko Dar es Salaam na mikoani.
Alisema Sh bilioni 8.1 zimetengwa kwa ajili ya kukodisha vichwa kutoka nje ya nchi, lakini akasema kuwa wamechukua sehemu ya fedha hizo kwa ajili ya kufanya ukarabati wa injini na mabehewa ambayo yatakuwa yanatoa usafiri kwa treni itakayokuwa inatoa huduma jijini Dar es Salaam.
"Zimebaki Sh bilioni 5.1 kwa ajili ya kukodi vichwa kutoka nje ya nchi, lakini hawa ambao tumewaomba kutukodishia wanaamini kuwa sisi ni vichwa vya wendawazimu nadhani hatutaweza kukodi tena hivyo vichwa badala yake tuwawezeshe wafanyakazi wetu wakarabati hivi vilivyopo," alisema waziri huyo.
Dk Mwakyembe alisema wakodishaji hao wametoa bei ya Sh milioni 3 kwa siku kwa ajili ya kukodisha kichwa kimoja, gharama  ambazo ni kubwa kuliko zile ambazo Rites ambao ni wawekezaji wa zamani ndani ya TRL ambao walikuwa wanakodisha kichwa kimoja kwa Sh
milioni moja kwa siku.
"Huu ni uwendawazimu kuendelea kukodi vichwa hivi na kama wanang'ang'ania nawasihi achaneni nao na tufufue vichwa vilivyopo kwa kutumia hiyo pesa iliyopo," alisema Dk Mwakyembe.
Pamoja na mafanikio hayo, Dk Mwakyembe amewaeleza wafanyakazi hao kuwa ndani ya TRL kuna tabia mbaya ya wizi na udokozi pamoja na hujuma mbalimbali mambo ambayo alisema yanamtia kichefuchefu.
Mtendaji Mkuu wa TRL, Kipallo Kisamfu alikiri kuwa mafuta ndio yanachukua kiasi kikubwa cha fedha kwani hesabu zinaonesha kuwa asilimia 70 ya matumizi ya TRL yanaenda kwenye mafuta kila mwezi.
Aliahidi kuwa watafanya kazi kwa bidii kwa ajili ya kusaka mitaji ya maendeleo kwa kampuni hiyo ambayo kwa sasa inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 baada ya kuondolewa wawekezaji wa Rites kutoka India.

No comments: