'JUMUIYA YA UAMSHO INATUMIWA NA WAHUNI ZANZIBAR'...

Polisi wakikabiliana na wafuasi wa kundi la Uamsho katika moja ya mitaa ya mjini Unguja.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imesema wakati kuna madai kwamba Jumuiya ya Uamsho ni ya kidini (Kiislamu), lakini imekuwa ikitumiwa na makundi ya wahuni ambayo yamejipachika majina tofauti.
Taarifa ya Tume hiyo iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana ikiwa imesainiwa na Kamishna wake, Zahor  Khamis, imetaja baadhi ya majina ya makundi hayo kuwa ni Mbwa mwitu, Simba mkali,  Ubaya ubaya na Toto tundu na kuongeza kuwa yamekuwa yakitumika kufanikisha azma yao.
Mbali na jumuiya hiyo kutumiwa na wahuni, Tume pia imesema kutekwa kwa kiongozi wa jumuiya hiyo, Shekhe Farid Hadi Ahmed, kuna utata mkubwa ambao unahitaji uchunguzi na ufafanuzi kufahamu huko alikotekwa na kutoa mfano wa madai ya kunyimwa kula kwa siku tatu bila kuathirika kiafya.
Tume hiyo imehoji kama kweli alikuwa ametekwa, aliwezaje  kufika msalani ambako alikuwa akinywa maji, wakati alikuwa amefungwa kitambaa usoni na mikononi akiwa na pingu na ilikuwa nyumba ambayo haijui!
Kutokana na utata huo, Tume imemtaka Shekhe Farid  kutoa maelezo yanayothibitisha pasipo shaka ili kuwathibitishia Wazanzibari, Watanzania na ulimwengu kwa jumla, juu ya kutoweka kwake.
“Shekhe Farid amedai alitekwa na watu wasiojulikana tarehe 16 mwezi huu na kuonekana siku tatu baadaye akiwa katika hali ya uzima na salama, jambo ambalo lilisababisha vurugu kubwa Zanzibar na kusimama kwa shughuli zote za kiuchumi na kijamii,” ilieleza taarifa hiyo ya Tume.
Kwa mujibu wa Tume, kutokana na fujo hizo zilizotokea, hasara ilitokea ambayo mpaka sasa haijajulikana thamani, askari Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Said Abdulrahman kuuawa.
Kutokana na matukio hayo, Tume imeishauri Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kuwatafuta na kuwakamata wote walioshiriki katika vurugu hizo na kuvunja vikundi vyote vya kihalifu vilivyoanza kushamiri Zanzibar.
“Tunalaani mauaji ya askari Abdulrahman kwani ni uvunjaji wa haki za binadamu, inapingana na sheria za nchi na ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 14 inayozungumzia haki ya kuishi na Katiba ya Zanzibar ibara ya 13 inayozungumzia haki ya kuwa hai,” taarifa hiyo ilifafanua.
Tume pia imelaani kitendo  alichofanyiwa Diwani wa CCM Wadi ya Chumbuni kwa kushambuliwa na kujeruhiwa, kitendo ambacho kinakwenda kinyume na haki za binadamu na Katiba ya Tanzania  inayopiga marufuku mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au adhabu za kumdhalilisha.
“Kuna uhusiano gani wa kutekwa kwa kiongozi wa Uamsho na  hujuma za mali za watu na CCM?” Taarifa hiyo ilihoji.
Kwa mujibu wa Kamishina wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa Polisi inafanya uchunguzi wa kina kubaini kama Shekhe Farid anahusika na mtandao hatari wa ugaidi wa Al-Qaeda.
Akizungumza kwa simu jana, Mussa alisema Polisi nchini inafanya kazi hiyo kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa ikiwamo Polisi - Interpol.
“Jeshi la Polisi nchini kwa sasa linafuatilia kwa karibu sana nyendo zote za kiongozi wa Uamsho Shekhe Farid ikiwamo kuhusishwa kwake na mtandao wa Al-Qaeda,” alisema.

No comments: