POLISI WASHUSHA BENDERA YA KUNDI LA UAMSHO ZANZIBAR...

Mmoja wa wafuasi wa Uamsho akionesha bendera ya kundi hilo.
Baada ya kuchoshwa na vitendo vya kihuni vinavyofanywa visiwani hapa, Serikali imeamua kusafisha vigenge hivyo ikiwa ni pamoja na kushusha bendera za Jumuiya ya Uamsho zilizokuwa zikipepea katika maeneo mbalimbali mitaani mjini hapa.
Kazi hiyo inafanywa na Jeshi la Polisi ambalo limethibitisha kusaka vikundi hivyo vya kihuni ambavyo vimekuwa vikijipachika majina mbalimbali kwa kutumia mwavuli wa Jumuiya hiyo kufanya fujo.
Akizungumza kwa simu jana, Kamishna wa Polisi, Musa Ali Musa, alisema polisi wamekuwa wakifanya msako dhidi ya vigenge vya vijana wanaofanya uhalifu na kuhatarisha amani na utulivu wa nchi.
“Jeshi la Polisi linachokifanya ni kutafuta vigenge vinavyofanya uhuni na kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria … tumeanza kuwabaini baada ya kutumia teknolojia kupitia video,” alisema Musa.
Alisema baadhi ya vijana wameanza kukamatwa baada ya picha zao kuonekana kwenye maandamano  ya Jumuiya ya Uamsho wakiwa na mapanga huku wakitoa kauli za ‘Chinja! Chinja’!
“Polisi haifanyi kazi kwa kukiuka misingi ya haki za binadamu … tunawafuata wahusika wa fujo baada ya kuwatambua,” alisema Kamishna Musa.
Taarifa zilizopo zilisema zaidi ya bendera 50 ziliteremshwa katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya Bububu, Mboriborini na Daraja bovu.
Aidha, ulinzi mkali na msako vinaendelea katika maeneo kadhaa ya mji ikiwa ni pamoja na Bububu ambako aliuawa askari Said Abrahman kwa kushambuliwa na watu wasiojulikana wakamjeruhi na kusababisha mauti yake.
Hivi karibuni, Jeshi la Polisi lilionesha picha za baadhi ya vijana wakiwa mstari wa mbele kwenye maandamano ya Jumuiya ya Uamsho, huku wakiwa na mapanga na Polisi kuomba msaada kwa wanaowajua kutoa taarifa ili kufikishwa kunakohusika.
Akihutubia Baraza la Iddi mjini hapa, Rais Ali Mohamed Sheni alisema uvumilivu wa Serikali sasa  umefika kikomo na kuongeza kwamba vyombo vya Dola vitachukua hatua kali dhidi ya watakaobainika kuvunja sheria za nchi huku akisisitiza hakuna aliye juu ya sheria.
Jumuiya ya Uamsho imeingia katika matatizo na Serikali baada ya wafuasi wake wakiongozwa na Shekhe Farid Hadi Ahmed, kutokana na kufanya maandamano na vurugu.

No comments: