WAZIRI WA NISHATI AIPIGA 'STOP' EWURA KUPANDISHA UMEME...

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameagiza Mamlaka ya Nishati na Maji nchini (EWURA), kutopandisha bei ya umeme kwa kuwa Serikali inalipa baadhi ya gharama za ufuaji umeme kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Akizungumza katika kipindi cha Dakika 45, kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV Dar es Salaam juzi, Profesa Muhongo alisema  badala ya kupandisha bei ya umeme, Serikali imeshusha gharama za kuunganisha umeme ili wananchi wengi wanufaike, kwani nishati hiyo si anasa bali ni huduma inayotakiwa.
“Hivi kama Serikali inatoa fedha za kuendesha mitambo ya kufua umeme, sasa Tanesco wanataka kupandisha bei ya umeme kwa mantiki gani, na wanazipeleka wapi hizo fedha?” Alihoji Waziri Muhongo.
Alifafanua kwamba Serikali inatoa fedha kufanya kazi hiyo kwenye mitambo ya kufua umeme nchini, hivyo hakuna sababu ya kupandisha bei ya umeme na kwamba hata madeni ya Tanesco ya mafuta ya mitambo hiyo yameanza kulipwa na Serikali.
Kuhusu mgao wa umeme, Profesa Muhongo alisema hakuna mgao wa umeme nchini na hautakuwapo na masuala ya umeme wa dharura pia hayatakuwepo tena na kusisitiza, kuna baadhi ya watu wanafurahia mgao kwa sababu binafsi zikiwamo za kisiasa na biashara.
“Niwaambie Watanzania, kwamba hakuna mgawo wa umeme na hautakuwapo, haya mambo ya umeme wa dharura nayo hayapo tena, ila kuna watu wanafurahia uwepo wa mgawo na hiyo ni kwa sababu zao binafsi zikiwamo siasa na biashara,” alisema Profesa Muhongo.
Alisema Watanzania wamechoka kuishi maisha ya karne ya 16, ilhali wapo karne ya 21, ya Sayansi na Teknolojia na kusisitiza, kwamba ni lazima wananchi kwenye maeneo yote nchini wapate umeme ili kuleta maendeleo.
“Hatuwezi kuendelea kama  nishati ya umeme haitafikia wananchi wengi, hivi sasa watumiaji wa nishati ya umeme nchi nzima ni asilimia 18.4 na vijijini ni asilimia 6.6, hii si sahihi ni lazima umeme usambae vijijini na nchi nzima,” alisema Profesa Muhongo.
 Alitaka Watanzania wasiwe na hofu ya umeme, kwani mpango wa wizara kwa miaka mitano ijayo ni kuhakikisha ifikapo 2015, umeme utakaozalishwa utaongezeka hadi megawati 2,780 kutoka za sasa ambazo ni 1,438.24
Kwa mujibu wa  Profesa Muhongo, hivi sasa matumizi ya umeme ya juu nchini ni megawati 830 na kiwango hicho cha matumizi hakijawahi kufikiwa kwa muda mrefu isipokuwa miezi miwili iliyopita ambapo yalifikia megawati 850.
Kuhusu kufikia lengo la kuzalisha megawati 2,780, alisema hilo linawezekana, kwa kuwa anaamini ana uwezo wa kulitekeleza na kwamba wizara anayoiongoza  ni moja ya fani zake na tayari wameanza kuongeza vyanzo vya kuzalisha umeme.
“Umeme tunaotumia sasa asilimia 65, umetokana na gesi asilia na tunatarajia pia kuzalisha umeme kutokana na makaa ya mawe ya Ngaka,” alisema Profesa Muhongo.
Alisema tatizo kubwa la awali la mgao wa umeme lilitokana na miundombinu ya Tanesco kuchoka na   hujuma na wizi wa miundombinu ya shirika hilo.
Profesa Muhongo alisema hata kama umeme ungezalishwa mwingi usingesafirishwa, kwa kuwa miundombinu iliyopo imechoka, hivyo katika mpango wa miaka mitano wa wizara hiyo, miundombinu ni eneo mojawapo linalofanyiwa kazi.
Alisema, ikiwa umeme utakatika ghafla, alishaagiza mameneja wa Tanesco kwenye kanda mbalimbali nchini kuomba radhi Watanzania kupitia vyombo vya habari na kueleza kwa nini jambo hilo limetokea.
Aliongeza, kuwa kama kuna matengenezo yanafanyika kwenye maeneo fulani na inabidi umeme ukatwe, ni lazima taarifa zitolewe kwa wananchi kupitia vyombo vya habari zikielewa ni maeneo gani hayatakuwa na umeme na kwa muda gani na sababu zipi.
Akizungumzia uchimbaji mafuta, gesi na urani, Profesa Muhongo alisema kuna upotoshaji mkubwa kuhusu rasilimali hizo na kwamba upotoshaji unachochewa na watu waliohudhuria mafunzo ya wiki moja kuhusu gesi na urani.
“Wapo wapotoshaji wakubwa wanaojidai kuwa mabingwa wa gesi na urani, si kweli, wamehudhuria mafunzo ya wiki moja na kupewa vyeti vya mahudhurio, sisi hatushindani nao, tunatumia wataalamu wetu wenye vyeti vya kitaaluma,” alisema Profesa Muhongo.
Kuhusu kugawa vitalu vya utafiti wa mafuta na gesi kwa wawekezaji, alisema si jambo geni kwenye sekta hiyo na tangu uhuru kuna mashimo 53 yaliyokwishachorongwa kwa ajili ya kuangalia kama kuna gesi au mafuta ardhini.
Alisema kitaaluma ni lazima utafiti wa mafuta au gesi ufanyike ikiwamo uchorongaji na kutaka wapotoshaji wanaosema wanajua masuala ya gesi na urani  waache, kwa kuwa mambo haya yanaendeshwa kitaalamu.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), ni lazima lisukwe upya ili liendane na hali ya sasa na kuwa na kampuni ya kizalendo itakayofanya utafiti wa gesi na mafuta badala ya kuziachia kampuni binafsi za nje kufanya kazi hiyo.

No comments: