LORI LAUA WATU WATATU HUKU MWINGINE AKINYONGA MTOTO NA KUJIUA...

Kamanda wa Polisi Dodoma, Zelothe Steven.
Watu watano wamefariki dunia mkoani Dodoma kutokana na matukio mawili tofauti likiwemo la mwanamume kunyonga mtoto wake  na kisha kujiua na ajali ya lori iliyosababisha vifo vya watu watatu na wengine 40 kujeruhiwa.
Akizungumzia matukio hayo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Steven alisema kuwa, mkazi wa Bicha Wilaya ya Kondoa Michael Jerome (43) alimuua binti yake Filomina Michael mwenye umri wa miaka mitatu kwa kumnyonga na kipande cha kitenge chumbani kisha na yeye kujinyonga kwa kutumia kitenge hicho hicho.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Oktoba 29, mwaka huu saa nne asubuhi
kijijini hapo ambapo chanzo cha mauaji hayo kinadhaniwa kuwa ni mgogoro wa ndoa baina yake na mkewe ambaye walikuwa wametengana tangu mwaka jana na alikuwa akihitaji kufika nyumbani kwa wakwe zake kwa ajili ya kikao cha usuluhishi.
Hata hivyo kamanda Zelothe alisema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea
kufuatilia uchunguzi zaidi wa tukio hilo la kinyama.
Katika tukio la ajali Kamanda Zelothe alisema kuwa, watu watatu wamefariki dunia huku wengine 40 kujeruhiwa baada ya gari la Jeshi lenye namba T.5747 JW09 aina ya Iveco likitokea kwenye msiba Kondoa mkoani hapa kuelekea Jijini Dar es Salaam kupinduka.
Ajali hiyo ilitokea juzi mchana katika Kijiji cha Zoisa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma kwenye barabara ya Dodoma Kiteto.
Alisema  gari hilo mali ya JWTZ Kikosi cha 312 cha Lugalo Jijini Dar es Salaam lilipinduka kutokana na mwendo kasi wa dereva Koplo Selemani Shija (40) ambaye alishindwa kulimudu gari wakati likiwa kwenye mteremko na kupinduka.
Waliofariki katika ajali hiyo wametajwa kuwa ni Thomas Degela anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 38 hadi 40, Zinduna  Khalfani anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25 na 30 ambao makazi yao hayafahamiki na Mariam Omary (24), mkazi wa Mondo Kondoa.
Kamanda Zelothe alisema kuwa katika ajali hiyo watu 34 walijeruhiwa akiwemo dereva wa gari hilo ambalo majeruhi watatu kutokana na hali zao kuwa mbaya walihamishiwa katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu.
Aliwataja majeruhi hao kuwa ni Maria Pascal (30),  Pendo Pascal (33), Mkazi wa Jijini Dar es Salaam na  Rajab Hassan (22), mkazi wa Manyoni Singida.
Kamanda Zelothe alisema  majeruhi 25 wamelazwa katika hospitali ya Serikali ya Wilaya ya Kongwa wakiendelea na matibabu.
Aliwataja watu hao kuwa ni Koplo Shija, Ayub Salum, Salum Kajelele, Akida Muhehe, Hamisi Bakari, Adam Ramadhani,  John Pascal, Elisha Mahaki, Mohamed Hussein,  Sikitu  Abdallah,  Zuhura Lameck, Rehema Idd (35) na  Rukia Masudi.
Wengine ni  Salma Ramadhani, Zuhura Abasi, Arafa Shabani, Stahimily Masudi, Hafsa Kijuu, Leah Jonas, Anastazia Pascal, Aliza Ally, Elizabeth Agustino, Hadija Ibrahim na Halima Hassan.
Pia majeruhi sita walitibiwa katika kituo cha afya cha Mkoka Wilaya ya Kongwa na kuruhusiwa ambao ni Husna Kavina, Asha Idd, Yassin idd, Nadia Muhagi, Mariam Daimeshi na Hussein Njenha.

No comments: