MKE AMUUA MUMEWE SABABU YA SANGARA...

Samaki aina ya Sangara.
Mkazi wa Kitongoji cha Nyasura, Latifa Masanja (21)  amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara akikabiliwa na mashitaka ya kumwua mumewe Mwita Marwa (28) kwa kumchoma kisu tumboni.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Safina Semfukwe, Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Masoud Mohamed alidai jana kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Oktoba 10 saa nane mchana.
Mohamed alidai kuwa chanzo cha ugomvi huo, ni  shinikizo la Marwa kwa mkewe awapikie samaki   aina ya sangara aliokuwa amewaleta, kazi ambayo Latifa alikataa kuifanya.
Alidai kutokana na shinikizo hilo lililoonekana kumkera Latifa, anayedaiwa kutowapenda samaki hao,  mke huyo alimparamia mumewe aliyekuwa hana habari na kumchoma kisu tumboni na kumsababishia kifo papo hapo.
Mohamed alidai kuwa baada ya mauaji hayo, mshitakiwa alijaribu kutoroka lakini alikamatwa na majirani waliomfikisha Kituo cha Polisi mjini hapa.
Hata hivyo, mshitakiwa hakutakiwa kujibu lolote kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kisheria wa kusikiliza mashitaka ya mauaji na alirejeshwa rumande hadi Oktoba 29 kesi yake itakapotajwa.

No comments: