MFUMUKO WA BEI WASHUKA KWA ASILIMIA 1.4...

Wafanyabiashara wakishusha nafaka sokoni jijini Dar es Salaam.
Mfumuko wa bei nchini hususani katika bidhaa za vyakula imeshuka kwa asilimia 1.4 katika kipindi cha Septemba ikilinganishwa na mwezi uliopita.
Akizungumza Dar es Salaam juzi kuhusu fahirisi za bei za kitaifa za Septemba, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephraim Kwesigabo, alisema kasi ya mfumuko huo imeshuka kutoka asilimia 14.9 ya Agosti hadi 13.5 Septemba mwaka huu.
Kwesigabo alisema kupungua kwa mfumuko huo wa bei katika kipindi cha Septemba, kunamaanisha kuwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma imepungua ikilinganishwa na hali ilivyokuwa Agosti.
Alisema katika fahirisi hiyo, imeonesha kuwa mfumuko wa bidhaa za vyakula majumbani na katika migahawa, imepungua kutoka asilimia 15.8 Septemba ikilinganishwa na asilimia 18.5 ya Agosti mwaka huu.
Pia alisema mfumuko wa bei hizo nchini umepungua ukilinganisha na nchi za jirani za Uganda ambayo mfumuko wa bei umepanda kwa asilimia 5.9 kutoka 5.4 na Zambia ambayo mfumuko wake umepanda kutoka asimilia 6.6 hadi kufikia 6.4.

No comments: