BAADA YA KIMYA KIREFU, DECI YAIBUKIA MAHAKAMANI KISUTU...

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kusimamia na Kuendesha Upatu (Deci), Mchungaji Jackson Mtares amekiri kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) iliwakataza kupokea fedha kutoka kwa mwanachama yeyote wa taaasisi hiyo.
Mtares alieleza hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati akitoa ushahidi katika kesi ya kuendesha shughuli za upatu bila kibali inayomkabili pamoja na wakurugenzi wenzake wanne.
Akihojiwa na Wakili wa Serikali Prosper Mwangamila, Mtares alidai katika barua ya majibu ya kuomba leseni ya kufanya shughuli za taasisi hiyo, BOT iliwatakaza kupokea fedha kutoka kwa mwanachama yeyote iwe kwa hiari au kwa lazima.
Hata hivyo alipoendelea kuhojiwa na kupewa barua hiyo ambayo imepokelewa mahakamani hapo kama kielelezo cha upande wa mashitaka, Mtares alidai kuwa Mkurugenzi mwenziye ambaye pia ni mshitakiwa ndiye atakayetoa maelezo zaidi.
Awali Mtares aliwasilisha kielelezo ambacho ni barua ya maombi waliyoandika kwa Gavana wa Benki Kuu (BOT) kuomba leseni ya kufanya shughuli za taasisi ambazo ni kusaidia watu wenye kipato cha chini kujikimu kimaisha.
Akiongozwa na Wakili wake wa utetezi Hudson Ndusyepo, Mtares alidai hakuhusika kupokea fedha wala kutoa risiti kwa wanachama na hata katika ushahidi uliotolewa mahakamani na upande wa mashitaka hakuna shahidi aliyedai yeye alipokea fedha.
Mtares aliendelea kudai kuwa,  Benki ya Afrika (BOA) ilikataa kuhifadhi fedha za taasisi hiyo hivyo walizihamishia katika akaunti ya kanisa lake la Jesus Christ  deliverance iliyopo katika Benki ya Wananchi Dar es salaam (DCB) ambayo ilikutwa na zaidi ya Sh bilioni 1.3 baada ya shughuli za Deci kusimama.
Alipoulizwa sababu za benki hiyo kukataa kuhifadhi fedha hizo alidai hajui bali walipewa taarifa kuwa wanatakiwa watoe fedha hizo haraka ndipo bodi ya wakurugenzi ilipoamua fedha hizo ziwekwe kwenye akaunti ya kanisa lake.
Aliendelea kudai kuwa wanachama walikuwa wanalipa kiingilio cha Sh 30,000 na baadaye wanaweka fedha na kupata uwezeshwaji (riba) ya asilimia 150 ya fedha ambayo mwanachama ameweka.
Alipobanwa kwa maswali na upande wa mashitaka, Mtares alidai fedha za riba  zilitokana na fedha walizokuwa wanaweka wanachama kwasababu Deci ilikuwa haijishughulishi na biashara yeyote zaidi ya kuwasaidia watu wenye kipato cha chini.
Hakimu Stewart Sanga aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 8 mwaka huu, wakatakapoendelea kusikiliza ushahidi wa upande wa utetezi.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Wachungaji wa makanisa tofauti ya Pentecoste ni, Dominic Kigendi, Samuel Mtares, Timotheo Ole Loitingye na  Arbogast Francis.
Wanadaiwa katika tarehe tofauti mwaka  2007 na  Machi 2009 katika Makao Makuu ya Deci, Mabibo Dar es Salaam walikusanya fedha kutoka kwa wananchi  wakiwaahidi kuwa watapata faida ya riba kubwa, katika mpango huo waliouita kupanda na kuvuna pia walifanya shughuli hiyo bila leseni.

No comments: