AJALI ZA BARABARANI ZAUA WATU NANE...

Kamanda Evarist Mangala.
Watu wanane wamekufa papo hapo na wengine 27 kujeruhiwa baada ya magari waliyokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso katika kijiji cha Kolandoto mjini Shinyanga.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Polisi mkoani hapa jana, ajali hiyo ilitokea saa 3.10 asubuhi katika barabara ya Shinyanga-Mwanza.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Evarist Mangala, alisema magari yaliyohusika na ajali hiyo ni pamoja na basi dogo namba T 914 DSD aina ya Mercedes Benz lililokuwa likiendeshwa na Nassib Said (42) wa Maganzo na lingine aina ya Mitsubishi Fuso lnamba T 650 APS likiendeshwa na Nazet Kiondo (45), mkazi wa Musoma, Mara.
Alisema ajali hiyo ilitokea wakati basi hilo dogo lililokuwa likitoka Maganzo kuja mjini hapa kuingia barabara kubwa na kugongana na lori hilo lililokuwa likitoka Mwanza pia kuja hapa na kusababisha vifo hivyo na majeruhi 17 kulazwa katika hospitali ya misheni ya Kolandoto.
Kamanda Mangala alitaja waliopoteza maisha katika ajali hiyo kuwa ni Leonard Nyabwinyo (19) mwanafunzi wa kidato cha tatu na Malick Denny (15) wa kidato cha kwanza sekondari ya Shinyanga.
Wengine ni Jacob Kitale (55) mwalimu wa sekondari ya Songwa, Mussa Abdallah (30), Violet Wilson (51), Hussein Bakari (35), Sudi Emmanuel (40) ambao wote ni wakazi wa Maganzo na mvulana anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 12 ambaye bado hajatambuliwa.
Madereva hao wanashikiliwa na Polisi na chanzo cha ajali bado kinachunguzwa.

No comments: