TAARIFA KAMILI YA VURUGU MKUTANO WA CHADEMA IRINGA HII HAPA...

Askari Polisi wakipita mbele ya nyama zilizonyofoka kutoka mwilini mwa mmoja wa waathirika katika vurugu zilizozuka kwenye mkutano wa Chadema katika Kijiji cha Nyololo, wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa.
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC), Daudi Mwangosi, amekufa katika vurugu za kuwatawanya wafuasi wa Chadema katika Kijiji cha Nyololo, Mufindi, Iringa.
Mwangosi ambaye ni mwakilishi wa Kituo cha Televisheni cha Chanel Ten mkoani Iringa, alifariki akiwa mikononi mwa polisi ambapo inadaiwa kabla ya kifo hicho, mwandishi huyo na mmoja wa maofisa wa polisi aliyekuwa amemshikilia, walilipukiwa na kitu kilichowajeruhi vibaya.
Akisimulia tukio hilo, mmoja wa mashuhuda aliyekuwepo katika mkutano hiyo ya Chadema, alidai kuwa kabla ya kufikwa na mauti, Mwangosi alikuwa katika majibizano na askari polisi.
Kwa mujibu wa madai ya shuhuda huyo, kabla ya kuanza kwa vurugu hizo, viongozi wa Chadema na wafuasi wake walikuwa katika mkutano wa kufungua tawi la chama hicho katika kijiji hicho.
Alidai kuwa wakiwa eneo la tukio, polisi walifika katika tawi hilo na kuwataka wafuasi wa chama hicho kutawanyika kwa kuwa mikutano ya vyama vya siasa imepigwa marufuku kupisha kazi ya Sensa ya Watu na Makazi ambayo imeongezewa siku saba baada ya muda wake wa awali kukamilika
Kutokana na amri hiyo, mtoa habari alidai kuwa wafuasi hao walikataa kutawanyika na kuwalazimu polisi kutumia mabomu ya machozi kwa ni ya kuwatawanya.
Wakati wakipiga mabomu hayo, inadaiwa mwandishi mmoja wa habari (jina limehifadhiwa), aliwafuata polisi na kuhoji sababu za kutumia nguvu hiyo kutawanya wananchi.
Mtoa habari huyo alieleza mwandishi huyo alikamatwa na kusababisha Mwangosi kwenda kujaribu kumnasua mwandishi mwenzake kutoka mikononi mwa polisi.
Shuhuda huyo alidai kuwa polisi walimsihi Mwangosi aondoke katika eneo hilo ili waendelee na kazi yao na alipokaidi, walimkamata na yeye.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo, wakati Mwangosi akiwa amezungukwa na askari polisi wanaokaribia watano, kulisikika mlio wa mlipuko na baadae Mwangosi na mmoja wa askari aliyekuwa amemshika walianguka chini.
Inadaiwa Mwangosi alifariki papo hapo baada ya kujeruhiwa vibaya katika mlipuko huo huku askari polisi huyo anayedaiwa kuwa wa cheo cha juu, akikimbizwa hospitalini baada ya kujeruhiwa vibaya pia.
Alipoulizwa Mhariri Mkuu wa Chanel Ten, Dina Chaali ambaye alikiri kupokea taarifa za kifo cha Mwangosi lakini hakuwa tayari kuzungumza chochote kuhusu kifo hicho.
Dina alisema baada ya kupata taarifa hiyo, wamelazimika kuwa na mkutano wa dharura na uongozi wa juu wa kituo hicho na baada ya hapo ndipo watatoa tamko.
Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Michael Kamuhanda alipopigiwa alisema yuko katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Iringa asingeweza kuzungumza wakati huo.
Hii ni mara ya tatu kutokea vifo katika vurugu zilizotokana na Chadema kukaidi amri halali za Polisi. Mara ya kwanza mkoani Arusha, watu wawili walikufa wakati wa vurugu za kutawanywa kwa wafuasi wa Chadema waliokuwa wamezuiwa kuandamana.
Hivi karibuni, mwishoni mwa mwezi uliopita, Chadema katika mikutano hiyo ya vuguvugu la mabadiliko katika Mkoa wa Morogoro, walikaidi amri ya kusitisha mikutano hiyo na kusababisha vurugu zilizozua kifo cha mwananchi mmoja aliyekuwa akijishughulisha na uuzaji wa magazeti.
Hata hivyo baada wa kifo hicho, Chadema walisitisha mikutano hiyo ili kuruhusu kumalizika kwa shughuli za Sensa ya Watu na Makazi ingawa mwanzoni walikaidi.
Mbali na kusitisha mikutano hiyo, Chadema walisisitiza kuwa muuza magazeti huyo aliuawa kwa risasi na Polisi jambo ambalo lilipingwa na taarifa ya daktari aliyemfanyia uchunguzi, ambayo iliweka wazi kuwa kifo hicho kilisababishwa na kupigwa na kitu kigumu kichwani.

No comments: