SIRI MPYA ZAFICHUKA MGOGORO WA KANISA LA MORAVIAN...


Mchungaji Clement Fumbo.
Sakata la mgogoro ndani ya Kanisa la Moravian Jimbo la Misheni Mashariki, Dar es Salaam, limechukua sura mpya baada ya baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Kanisa hilo kufichua siri, kwamba mgogoro huo umechangiwa na matumizi mabaya ya karibu Sh milioni 529, upotevu wa vyerehani 10, jenereta, kamera na upuuzwaji mkubwa wa vikao.
Vyanzo vya kuaminika vimesema kwamba vitendo hivyo ambavyo vinakiuka kanuni na taratibu za Kanisa hilo, vilikuwa vikifanywa na Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Jimbo hilo anayedaiwa kusimamishwa, Mchungaji Clement Fumbo.
Hata hivyo, alipozungumza hivi karibuni, Mchungaji Fumbo alikiri kuwapo mgogoro huo, lakini akasema hajakabidhiwa barua yoyote ya kusimamishwa uongozi na anaendelea kwenda ofisini kufanya kazi kama kawaida.
Pamoja na hilo, Mchungaji Fumbo alisema wapo watu wachache wenye nia ya kuharibu Kanisa hilo, lakini atasimama kidete katika ukweli na haki ya waumini.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili wiki hii, ziliweka bayana ukosefu wa maadili na upuuzwaji wa maelekezo ya uendeshaji Kanisa, ambao umesababisha kupotea kwa zaidi ya Sh milioni 529 za Kanisa. 
Pia mali zingine za Kanisa, vikiwamo vyerehani 10, jenereta na kamera za video vilivyokuwa kwenye Usharika wa Ukonga vimetoweka katika mazingira ya kutatanisha bila maelezo yoyote juu ya mali hizo.
Wakizungumza juzi, baadhi ya wajumbe wa halmashauri hiyo ambao hata hivyo waliomba majina yao yahifadhiwe, walisema wamelazimika kufanya hivyo ili kuondoa upotoshaji unaoendelea kufanywa na baadhi ya waumini na viongozi wa   juu ya mgogoro huo.
Pamoja na kueleza kilichotokea hadi  Mwenyekiti huyo akasimamishwa kazi, wajumbe hao wa halmashauri hiyo walisema suala hilo sasa litafikishwa kwenye mkutano wa chombo cha juu kabisa cha uamuzi - Sinodi,  ili kukata ‘mzizi wa fitina’, hatua inayodaiwa kuzua hofu kwa wahusika na kuanza kutapatapa.
“Hakuna sababu ya suala hili kukuzwa kupitia vyombo vya habari. Taratibu za Kanisa ziko wazi, vipo vikao vinavyotambulika kikanisa. Ipo Sekretarieti, ipo Halmashauri na Halmashauri Kuu ya Kanisa, vipo vikao vya usuluhishi na kipo kikao cha Sinodi,” alisema mmoja wa wajumbe hao wa halmashauri.
Akizungumzia upotoshwaji wa hatua zilizochukuliwa na Halmashauri Kuu ya Kanisa hilo za kumsimamisha Mwenyekiti Fumbo,  mjumbe huyo alisema ni baada ya kiongozi huyo wa Kanisa kukiuka taratibu za uendeshaji na kupuuza maelekezo ya vikao vyote ikiwamo Sinodi juu ya utekelezaji wa masuala mbalimbali ya Kanisa.
“Mara kadhaa Mwenyekiti amepuuza agizo la kumwajiri Mweka Hazina mwenye sifa kwa vile aliyepo sasa hana sifa hiyo, jambo ambalo ni hatari. Mwenyekiti amepuuza agizo la makao makuu kujengwa Chamazi Chanika na sasa anataka yajengwe Tabata.
Mwenyekiti amepuuza agizo la kufanyika kwa ukaguzi wa fedha na mali za Kanisa na kukataa kutoa ushirikiano kwa Tume iliyoundwa kikatiba tena chini ya ushauri wa vyombo vya juu kabisa.
Mjumbe mwingine wa halmashauri hiyo akizungumzia upotevu wa Sh milioni 529 za Kanisa, alisema hoja hiyo iliwasilishwa kwenye moja ya vikao halali vya halmashauri na viongozi wa juu,  wakiwamo wachungaji kutoka Jimbo mama la Kusini.
 “Baada ya hoja hii iliamuliwa iundwe Tume ichunguze kama kuna mazingira ya fedha kutumika vibaya ili baadaye aitwe Mkaguzi wa Nje kukagua na kutoa maelekezo. Mwenyekiti kwa sababu anazozijua baada ya kikao kile alikataa kuitambua Tume iliyoundwa kwa mujibu wa Katiba, maana Katiba inasema itaundwa Kamati (Tume) kuchunguza jambo.
“Wakati Tume inatakiwa ianze kufanya uchunguzi, yeye aliomba mwezi mmoja ajiandae, halafu wakati muda huo unakaribia kufikia mwisho, ghafla akaomba likizo ya miezi mitatu eti anakwenda masomoni,” alidai mjumbe huyo.
Mjumbe huyo alisema pamoja na majalada hayo kuondolewa, Tume hiyo ilifanya kazi yake kwa kuangalia vielelezo vingine vya matumizi ya fedha na kubaini kuwa Sh milioni 529 zimetumika bila kumbukumbu na vielelezo vya kutosha na pia mali za Kanisa kama vyerehani 10 vilivyonunuliwa, ili kuanzisha mradi wa ushonaji katika Usharika wa Ukonga na jenereta, kamera za video vimepotea na haijulikani viliko.
Wakizungumzia ukiukwaji wa kanuni, wajumbe hao walidai kufanywa katika maeneo tofauti kama vile kwa Mwenyekiti kukaidi agizo la vikao vyote vya Kanisa ilikiwamo Sinodi kumwondoa Mweka Hazina wa Kanisa hilo kutokana na kukosa sifa.
Vikao halali pia viliagiza  kuajiriwa kwa Mkaguzi wa Ndani, lakini amekataa kuajiri mkaguzi huyo, Mwenyekiti pia aling’ang’ania kubarikiwa ili kuwa Mchungaji,  Mweka Hazina huyo wa Kanisa wakati hajasomea uchungaji, suala lililoleta mgogoro mkubwa hadi Askofu akaamua kumbariki ili kuepusha balaa.
Wakizungumzia kuhusu suluhisho la mgogoro huo, wajumbe hao walisema kwa vile Mwenyekiti anakana kuhusika na tuhuma hizo, ni lazima sasa suala hilo lifikishwe kwenye Mkutano wa Sinodi ili kutafuta ufumbuzi kwa maslahi ya Kanisa.
“Sasa Sinodi itaitishwa ili suala hili likajadiliwe na uamuzi upatikane. Lakini kwa vile suala hili linapotoshwa kutokana na taarifa zinazochapishwa kwenye magazeti na waraka alioandika Mwenyekiti, ndiyo maana halmashauri ilimtuma Makamu Mwenyekiti Mchungaji Saul Kajula, kupita kwa Wakristo ili kulitolea ufafanuzi. Lengo hapa ni kujenga heshima ya Kanisa kwa kuona taratibu zinafuatwa.”
Kuhusu taarifa zilizotolewa na Katibu wa Umoja wa Mabaraza ya Wazee wa Jimbo hilo hilo, Nelson Ngajilo kwamba lipo kundi la watu lenye nia ya kumwondoa Mwenyekiti ili kuweka kiongozi wao  na kufanya biashara na Kanisa, wajumbe hao walipuuza suala hilo kwa madai kuwa linalenga kuchepusha hoja ya msingi ya matumizi mabaya ya fedha na ukiukwaji Katiba  na kuchanganya Wakristo.

No comments: