SABA WAFA KWA KUFUKIWA NA KIFUSI KWENYE MGODI LINDI...

Wasamaria na wachimbaji wakisaidia kutoa miili ya watu 
waliokufa kwa kufukiwa na kifusi kwenye mgodi huo juzi.
Watu saba wamekufa katika ajali ya kufukiwa na kifusi kwenye migodi ya Nandagala inayochimbwa madini aina ya change color garnet yaliyoko wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Akizungumzia ajali hiyo iliyotokea juzi saa nane mchana, Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Agness Hokororo alisema watu saba walikufa baada ya kufukiwa na kifusi wakati walipokuwa wakitafuta madini hayo.
Hokororo alisema wachimbaji hao walikuwa wanane kwenye shimo hilo na kati yao, mmoja wao aliokoka lakini alivunjika mguu baada ya kudondokewa na mwamba.
Aliwataja waliokufa ambao wameshachukuliwa na ndugu zao kwa maziko kuwa ni Uwesu Bakari (25), mkazi wa Rondo mkoani Lindi, Mohamed Omary (28) wa Morogoro na Bakari Liganga (26), mkazi wa Chunyu.
Wengine ni Adam Sayai wa Bunda, Rashid Yassin kutoka Nachingwea na wengine wawili waliojulikana kwa jina moja moja akiwemo Chakoda (20), mkazi wa Dar es Salaam na Nyang'ana (42) anayetokea Musoma.
Kutokana na ajali hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya, aliagiza machimbo hayo yafungwe na kuwataka wachimbaji hao kuondoka katika eneo hilo.
Akizungumza baada ya kutembelea eneo la ajali, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene aliagiza Ofisi ya Kanda ya Madini Mtwara, kufunga machimbo yote ambayo hayafuati utaratibu wa uchimbaji.
Katika agizo hilo, alitaka migodi yote ambayo wachimbaji wadogo wanatumia zana duni ifungwe. Alisema kuna umuhimu mkubwa kutoa elimu ya kutosha ya umuhimu wa zana za kisasa za kuchimbia madini, ili kuepusha vifo kama hivyo.

No comments: