MAJAMBAZI WAPORA MAMILIONI BENKI DAR...

Kamanda Suleiman Kova.
Majambazi jana walivamia Commercial Bank of Afrika (CBA), Tawi la Barabara ya Nyerere na kuiba mamilioni ya fedha zikiwamo fedha za kigeni.
Ingawa Polisi katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imesema mpaka sasa kiasi cha fedha kilichoibwa hakijafahamika, zipo taarifa kuwa fedha zilizoibwa ni zaidi ya Sh milioni 350 pamoja na fedha za kigeni aina ya Dola za Marekani na Euro.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, Suleiman Kova, Polisi kwa kushirikiana na Makao Makuu ya benki hiyo wanafanya uchunguzi ili kubaini kiasi halisi kilichoibwa zikiwamo fedha za kigeni katika benki hiyo iliyopo katika Jengo la Jamana.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kova alisema wizi huo ulifanyika kimya kimya hali inayofanya waamini kulikuwa na njama iliyopangwa na baadhi ya wafanyakazi wa benki hiyo.
"Majira ya saa 2.30 asubuhi, tulipokea taarifa kutoka katika tawi hilo kwamba kuna wizi uliotokea kimya kimya katika namna ambayo majirani na wapita njia nje ya tawi hilo hawakugundua kinachoendelea," alisema Kamanda Kova.
Alisema baada ya kupokea taarifa hiyo, polisi walifika katika eneo la tukio ambapo katika uchunguzi wao wa awali, waligundua kwamba kuna watu sita wasiofahamika waliofika katika tawi hilo tangu saa 12.45 asubuhi.
Kwa mujibu wa Kova, watu hao walipofika asubuhi hiyo, walimkuta Meneja wa tawi hilo, Victoria Munishi (47) na msaidizi wake, Baraka Sheshambo (40), wakiingia kazini na kumwita Meneja huyo kwa jina lake ambapo aliingia nao ndani.
Kova alidai kuwa baada ya kuingia nao ndani, wahalifu hao walitoa bastola na kuwalazimisha Munishi na Sheshambo anayeshughulikia huduma kwa wateja, kufungua mlango wa chumba cha kuhifadhia fedha pamoja na chumba maalumu kinachodhibitiwa na mitambo maalumu ya kuzuia wezi.
Alidai uchunguzi huo wa awali ulibaini wahalifu hao walikaa ndani ya benki hiyo kwa saa mbili bila taarifa hizo kufika polisi au makao makuu wa CBA, jambo ambalo si la kawaida katika taasisi kubwa za fedha.
"Zipo dalili za kutosha zinazoonesha kwamba kuna njama pamoja na ushirikiano kati ya wahalifu hao na baadhi ya watumishi wa benki hiyo, hivyo Jeshi la Polisi linawashikilia meneja wa tawi hilo, msaidizi wake na mlinzi wa zamu ya asubuhi," alisema Kamanda Kova.
Alisema mlinzi huyo wa Kampuni ya Security Group anashikiliwa kwa kutochukua hatua zozote hata pale alipogundua mmoja kati ya wahalifu hao, alikuwa amevaa kitambulisho cha CBA wakati si mtumishi wa benki hiyo.
Tayari msako mkali unaendelea ili kuwakamata wahalifu hao ambapo Kova aliwaomba raia wema kutoa ushirikiano, ili kufanikisha kupatikana kwa taarifa za wahalifu hao.
Pia Kamanda Kova alitoa mwito kwa wenye mali wote kuwa waangalifu na kuajiri watu waaminifu ili kuepuka matatizo ya wizi.

No comments: