SABA WAFA BAADA YA GARI KUSHINDWA KUPANDA MLIMA...

Watu saba wamekufa wakati gari walilokuwa wakisafiria liliposhindwa kupanda mlima na kupinduka.
Taarifa kutoka eneo la ajali zilieleza kuwa gari hilo maarufu chai maharage lilipofika katika Kijiji cha Rondo wilayani Lindi Vijijini, lilishindwa kupanda mlima, likarudi nyuma na kupinduka usiku wa kuamkia jana.
Akizungumza jana, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa ya Sokoine, Dk Nichalaus Mmuni, alithibitisha kupokea maiti hao na majeruhi kadhaa.
Alisema baadhi ya majeruhi walipelekwa Hospitali ya Nyangao kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya X-Ray ambavyo havipo katika Hospitali ya Mkoa.
Kwa mujibu wa Dk Mmuni, ajali hiyo ilitokea usiku kuamkia jana na taarifa zilipelekwa katika hospitali hiyo ili kutoa msaada wa gari la kuwasafirisha majeruhi na miili ya marehemu.
Kamanda wa Polisi mkoani Lindi, George Mwakajinga alithibitisha kutokea ajali hiyo katika Kijiji cha Rondo, wilayani Lindi.
Hata hivyo hakuwa tayari kuzungumza zaidi kuhusu ajali hiyo kwa kuwa alikuwa ametoka kukagua ajali hiyo na bado hajaandaa taarifa yoyote.
Baadhi ya mashuhuda walidai kuwa gari hilo lilikuwa likitokea Lindi Mjini kwenda Rondo wilayani Lindi Vijijini.
Walidai lilikuwa na abiria wengi na barabara siyo nzuri kutokana na kuwapo na vifusi na mawe mbele yake.
Kwa mujibu wa madai ya mashuhuda hao, dereva wa gari hilo ambaye hajajulikana alipoona kuna mawe yamepangwa mbele yake wakati yuko mlimani, alifunga breki ambayo ilifeli hatimaye lilirudi nyuma na kupinduka.

No comments: