MSICHANA AFARIKI BAADA YA KUANGUKIWA NA FREMU YA DIRISHA...

Msichana amekufa mbele ya mtaa wenye maduka juzi pale fremu kubwa ya dirisha ilipomdondokea kichwani wakati akipita mbele ya jengo hilo ambapo shughuli za ujenzi zilikuwa zikiendelea.
Upepo mkali uling'oa fremu na kumgonga msichana huyo aliyevalia nadhifu, anayedhaniwa kuwa ni mfanyakazi wa ofisini ambaye ana umri wa kati ya miaka 20 hivi.
Wapitanjia na wafanyakazi wa ujenzi katika jengo hilo linalokadiriwa kuwa na thamani ya mamilioni ya pauni lenye ghorofa sita kwa ajili ya ofisi, kando ya mtaa wa Oxford huko Central London, walipambana kujaribu kuokoa maisha ya msichana huyo lakini alithibitika kufa pale pale katika eneo la tukio.
Juzi usiku mashuhuda walidai dirisha 'zito sana' liliteleza kutoka kwenye ukuta na kuanguka chini ya jengo hilo, na kwamba vizuizi kwenye eneo la jengo hilo vimeondolewa hivi karibuni.
Ajali hiyo ilitokea majira ya Saa 5:30 asubuhi kwenye jengo la Hanover Square lililoko Mayfair, ambalo limepangishwa ofisi kadhaa za gharama sana mjini London.
Nyumba ya sanaa iko katika ghorofa ya chini na jengo la Vogue, makao makuu ya mchapaji Conde Nast, mkabala na jengo hilo.
Dario Motti mwenye miaka 65, alisema fremu yenye urefu wa futi 12 iliteleza kwenye ukuta kabla ya kumwangukia msichana huyo. "Niliona fremu ikipokelewa jana," aliongeza. "Zilikuwa nzito mno na kupandishwa kwa kutumia kreni."
Kohei Matsumoto, meneja wa mgahawa ulio karibu wa Itsu sushi, aliongeza: "Wenzangu wawili waliona msichana akikunja kushoto kuelekea Mtaa wa Hanover. Alikuwa akila ndizi.
"Kitu kilichofuatia walichoshuhudia ilikuwa fremu ya dirisha ikimwangukia kichwani. Hakupiga kelele, ilitokea haraka mno."
Mtu mmoja ambaye anafunga nyaya za umeme kwenye jengo la jirani, ambaye hakutaka kujitambulisha, alisema kwamba ilihitajika watu kumi kuweza kuondoa fremu ile katika mwili wa msichana huyo.
"Nilisikia mlio mkubwa wa kushangaza," alisema. "Niligeuka na fremu ilikuwa imeshatua chini. Nilikuwa natumaini haikuleta madhara, lakini baadaye nikaona mkono.
"Kulikuwa na mwanamke ambaye anasemekana alikuwa ni daktari.
"Macho yake yalikuwa wazi na nikashuhudia akizogeza mkono wake na kukata roho, na kisha akafumba macho, alikuwa keshakufa. Alikuwa sehemu mbaya katika muda mbaya."
Beverley Hazel, mkazi wa Kennington, South London, akiwa njiani kuelekea kazini majira ya Saa 5:30 asubuhi ndipo alipoona mwanamke kalala barabarani.
Alisema: "Alikuwa kijana sana. Nina mabinti wawili, mmoja ni mdogo na mwingine ni mkubwa kuliko mwanamke huyu."
Msemaji wa kampuni ya Westgreen Construction Ltd, wa Richmond-upon-Thames, Surrey, ambaye ni meneja wa mradi wa ujenzi wa jengo hilo, alisema: "Tutafanya chochote ambacho ni muhimu. Hii ni ajali mbaya sana."
Mwili wa mwanamke huyo, ambao ulifunikwa kwa turubai la njano la polisi, uliondolewa kwa gari binafsi la wagonjwa majira ya Saa 12:45 juzi jioni.
Mkuu wa Afya na Usalama alisema walikuwa 'wakikusanya taarifa za awali'. Msemaji wa Polisi Makao Makuu alisema juzi usiku kwamba uchunguzi ulikuwa 'unaendelea'.

No comments: