WATOTO WAMCHINJA BABA YAO KWA PANGA...

Vijana wawili wa kiume wanatuhumiwa kumchinja kwa panga baba yao mzazi usiku wa kuamkia Sikukuu ya Idd el Fitri kwa tuhuma za kumroga mama yao mzazi anayesumbuliwa na ugonjwa wa mapafu na kuvimba miguu.
Vijana hao ambao ni Nelson (37) na Cuthbert Mkini (28), wanadaiwa kumwua baba huyo, Ejid Mkini (65) Jumamosi saa 3.40 usiku nyumbani kwake, katika Kijiji cha Pomerin, Kilolo mkoani hapa.
Wakati Nelson ni mkazi wa kijiji hicho, Cuthbert ni mwanafunzi wa Chuo cha Ualimu Agafilo, wilayani Njombe.
Akisimulia alivyoshuhudia mauaji hayo, Roida Kivamba ambaye ni mke wa Nelson, alidai katika mazingira ya kutatanisha, mumewe na shemeji yake, walifika nyumbani kwa baba yao saa tatu usiku siku ya tukio.
Alidai walipofika walidai kuwa wamekwenda kumjulia hali mama yao mzazi anayeendelea kuugua. 
Baada ya kumjulia hali mama yao, alidai watuhumiwa hao waling’ang’ania kulala kwenye sebule ya nyumba hiyo yenye vyumba viwili vya kulala, uamuzi uliopingwa na baba yao.
Alidai zogo hilo lilihitimishwa kwa watuhumiwa hao kumpiga baba yao kabla ya kumchinja.
"Wakati wote wakifanya hivyo, nilijaribu kuwasihi wasifanye hivyo, huku nikipiga kelele za kuomba msaada kwa majirani lakini niliambulia kipigo kilichonifanya nikimbie mbali na nyumba kwa hofu ya kuuawa," alidai Roida.
Alidai aliporudi nyumbani akiwa na baadhi ya majirani, walikuta mzee huyo amekwishakufa huku watuhumiwa wakiwa wamekimbilia kusikojulikana.
Hata hivyo katika mazingira ya kutatanisha, baadhi ya wananchi wa kijiji hicho waliozungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina gazetini, walidai kupokea kifo cha mzee huyo kwa masikitiko, lakini wengine walifurahia.  
"Mzee huyu alikuwa mtaalamu kweli kweli wa mambo ya kishirikina na alikuwa kero kwa wananchi na familia yake, kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa na matatizo mengi ya watu ikiwa ni pamoja na magonjwa yanayomsumbua mkewe," alidai mmoja wao.
Kutokana na mauaji hayo Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Gerald Guninita aliuagiza uongozi wa Kijiji cha Pomerin kuendesha kura ya siri ili kubaini waganga wa kienyeji wanaopiga ramli.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Peter Kakamba alikiri kupata taarifa za mauaji hayo na kusema wauaji wanasakwa.

No comments: