MKURUGENZI MKUU BANDARI ASIMAMISHWA KAZI...

Mkurugenzi Mkuu Ephraim Mgawe
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amewasimamisha kazi vigogo saba wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), akiwamo Mkurugenzi Mkuu, Ephraim Mgawe kwa tuhuma za uhujumu uchumi na kukaidi maagizo ya Ikulu.
Tuhuma hizo ni pamoja na wizi wa kontena za wateja unaofanywa katika Kitengo cha Kontena (TICTS), udokozi wa mizigo na vitu mbalimbali vikiwamo vifaa vya magari, rushwa ndogo na kubwa na wizi wa mafuta katika kitengo cha KOJ.
Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe uamuzi wa kusimamishwa kazi kwa vigogo hao, aliufanya juzi baada ya kikao na Bodi ya Wakurugenzi ya TPA na kubaini kuwapo kwa vitendo viovu vinavyochangia kuhujumu uchumi wa nchi.
Vigogo hao walisimamishwa kazi kupisha uchunguzi utakaofanywa na Tume maalumu aliyoiunda.
"Wamesimamishwa kupitisha uchunguzi na ripoti ya Tume hii, ndiyo itakayotoa majibu kama wanahusika na ikibainika hawahusiki na tuhuma hizo watarudishwa kazini," alisema.
Pamoja na Mgawe, wengine waliosimamishwa kazi ni naibu wakurugenzi wakuu wawili wa TPA waliotajwa kwa majina moja moja ya Mfuko na Koshuma. Pia yumo Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Cassian Ng’amilo, Meneja wa Kurasini Oil Jetty, Meneja wa Jetty na Terminal Oil Engineer ambao hawakutajwa majina.
Dk Mwakyembe alisema kuwapo kwa vitendo hivyo ndani ya TPA, kumefanya wateja wa Malawi, Uganda, Zambia na Congo kuhama bandari hiyo kwenda bandari za Mombasa, Kenya; Durban, Afrika Kusini na Beira, Msumbiji, hali inayoyumbisha uchumi wa nchi.
"Wateja wanaona ni heri wahamie kwenye hizo bandari licha ya kuwa ziko mbali na nchi zao, lakini vitendo viovu vilivyoko TPA vimewachosha na Serikali haiwezi kukaa kimya juu ya vitendo hivi vya uhujumu uchumi vinavyoendelea katika bandari yetu," alisema Waziri Mwakyembe na kuongeza kuwa imani ya wananchi juu ya bandari hiyo imepungua.
Akichambua tuhuma hizo, alisema kuna wizi wa mafuta unafanywa KOJ kwa kisingizio cha kupakua mafuta machafu. Alisema yeye binafsi alishuhudia juzi alfajiri yakipakuliwa mafuta safi zaidi ya lita 26,000 katika lori na lingine likisubiri pembeni kupakua.
Alisema alishuhudia hata kwenye mafuta kuna lumbesa na katika uchunguzi, akabaini kuwa mafuta hayo yanaishia kuuzwa kwenye vituo vya mafuta kwa ajili ya uchakachuaji.
Hata hivyo, alisema katika kujiridhisha, alipeleka sampuli za mafuta hayo kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) na Mombasa, kufanya uchunguzi wa mafuta yanayodaiwa kuwa machafu.
"Ndiyo maana vita vya zabuni ya kupakua hicho kinachoitwa mafuta machafu ni sawa na vita ya tatu ya dunia, kwani inagombewa sana," alisema na kuongeza kuwa Kampuni ya Singirimo iliyopewa zabuni ya kufanya kazi hiyo inamilikiwa na vigogo wa TPA.
Alisema wizi huo unachangia upotevu wa mafuta kutoka melini hadi KOJ kwa asilimia mbili ya mafuta yanayoingia nchini kiasi ambacho ni kikubwa duniani kote wakati mafuta yanayotolewa Mashariki ya Kati yakiwa kwenye meli upotevu ni asilimia 0.5 tu.
Kuhusu Kampuni ya Singirimo, Dk Mwakyembe alisema tangu mwaka 2008 Ikulu ilitoa maelekezo kwa TPA kuwa kampuni hiyo haifai kufanya kazi bandarini hapo kwa vile inashiriki kuiba mafuta safi kwa kisingizio kuwa ni machafu. "Lakini kwa kuwa ni biashara ya viongozi wa juu wa TPA walikaidi agizo la Ikulu."
Alisema kampuni hiyo ameisimamisha kuendelea na kazi hiyo na kuiagiza Bodi ya TPA kuteua mzabuni mwingine kufanya kazi hiyo katika kipindi hiki ambacho uchunguzi utakuwa unafanyika.
Kuhusu TICTS alisema kuna upotevu mkubwa wa kontena za wateja hasa zenye vitenge, jambo ambalo alisema limezua malalamiko kutoka kwa wateja wa nchi jirani hali ambayo alisema imechangia wateja kuikimbia TPA.
Katika kushughulikia hilo, kwanza aliagiza wanasheria wa TPA kuchambua mkataba kati ya Serikali na TICTS kuona ni kiasi gani cha makubaliano kina manufaa kwa Taifa. Kazi hiyo itakamilika Jumatano wiki ijayo na watampelekea taarifa ili achukue hatua zaidi.
"Haiwezekani kontena lenye vitenge hata likilindwa na askari 20 pale TICTS ni lazima liibwe, hapa kuna tatizo na hii wateja kutoka nje ya nchi wamekuja kwangu kulalamika na imechangia wengi kuikimbia bandari yetu," alisema Dk Mwakyembe.
Dk Mwakyembe alisema Tume ya Uchunguzi ya watu saba aliyoiunda itafanya kazi kwa wiki mbili; hakutaka kutaja majina ya wajumbe wake kwa madai kuwa wanashughulika na watu wenye fedha nyingi; hivyo wanaweza kuwanunua iwapo watawabaini. Alisema tume hiyo imepewa hadidu za rejea zenye maswali 50 ambayo watahoji watu mbalimbali.
Waziri alisema ili uchunguzi huo ufanyike kwa haki, ni lazima watuhumiwa wote wawe nje ya ofisi zao na aliiagiza Bodi kuteua watu waadilifu na wachapa kazi kukaimu nafasi za maofisa waliosimamishwa.
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Dk Mwakyembe alimteua Madeni Kipande ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Barabara katika Wizara ya Ujenzi kukaimu nafasi ya Mgawe.
Dk Mwakyembe alisema aliiomba Bodi imruhusu ateue mtu kutoka nje akaimu nafasi hiyo kwa vile wa ndani ya TPA wanaweza kuogopa kushika wadhifa huo kutokana na hali ilivyo sasa.

No comments: