WANAMICHEZO SABA WA CAMEROON WAZAMIA UINGEREZA...

Wanamichezo saba kutoka Cameroon wametoweka katika hali ya utatanishi kutoka kwenye kijiji cha Olimpiki mjini London katika kile kinachoonekana juhudi za kuikimbia nchi yao na kuomba hifadhi ya ukimbizi nchini Uingereza
Mkuu wa msafara wa timu ya Cameroon alisema wanamichezo ambao ni pamoja na mabondia watano, muogeleaji na mwanasoka wote wana viza ambazo zitawaruhusu kubakia nchini Uingereza hadi Novemba, mwaka huu.
Mwanasoka ambaye ni kipa wa akiba katika timu ya wanawake aliyetajwa kuwa ni Drusille Ngako, alikuwa wa kwanza kutoweka na kufuatiwa na muogeleaji Paul Edingue Ekane.
Mabondia watano, Thomas Essomba, Christian Donfack Adjoufack, Abdon Mewoli, Blaise Yepmou Mendouo na Serge Ambomo walitoweka Jumapili iliyopita. Wote walikuwa tayari wameshatolewa mashindanoni.
Hii si mara ya kwanza kwa wanamichezo wa Cameroon kutoweka wakati wa michuano ya michezo ya kimataifa kwani wachezaji kadhaa walitoroka kutoka kwenye msafara bila taarifa katika michuano ya hivi karibuni kwenye Michezo ya Francophonie and Commonwealth.
Ofisi katika Wizara ya Mambo ya Ndani Uingereza inayohusika na uhamiaji haikuweza kusema chochote kama kuna mchezaji yeyote kati ya hao saba ambaye ameshaomba hifadhi ya ukimbizi.

No comments: