MBUNGE AHUSISHWA NA MAPIGANO MSIKITINI...

Wakati Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ukikaribia ukingoni, waumini wa Msikiti wa Jumuiya ya Sunni Muslim Jamaat uliopo Mtaa wa Mosco jijini Dar es Salaam, juzi walipigana na kusababisha vurugu ndani ya msikiti huo, huku baadhi yao wakijeruhiwa vibaya.
Chanzo cha vurugu hizo ambazo zinadaiwa kumhusisha Mbunge wa Mpendae, Salim Abdullah Turky (CCM), ni uchaguzi wa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya msikiti huo ambao mgogoro wake umedumu kwa muda mrefu na sasa upo mahakamani.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Imamu wa msikiti huo, Shehe Mohamed Khatri alisema vurugu hizo zilianza usiku mara baada ya kumaliza swala ya Tarawehe ambako kulitokea kutokuelewana na ghafla watu wakaanza kupigwa.
“Ndio tulikuwa tunajiandaa kusoma dua ya hitma baada ya kufiwa na wenzetu hivi karibuni, ghafla hali ilibadilika nilishtukia nimepigwa kibao na nilipoangalia pembeni niliona wenzangu wakipigwa hovyo na kundi la watu linalodaiwa kuongozwa na huyu Mbunge Turky,” alidai Khatri.
Alisema wakati vurugu hizo zikiendelea huku baadhi ya waumini wakipiga kelele, ghafla waliingia vijana wenye silaha na kuvamia msikiti na kusababisha eneo hilo kuwa la hatari ambapo watu takribani saba walijeruhiwa kwa kupata majeraha sehemu kadhaa katika miili yao.
Mmoja wa wazee wa msikiti huo, Shehe Majid Saleh alisema amesikitishwa na mapigano hayo ambayo yalisababisha waumini wa msikiti huo kukatishwa ibada yao huku watoto waliokuwa wakisoma Kurani wakinyang’anywa vipaza sauti na kufukuzwa nje.
“Kuna watu takribani saba wamejeruhiwa, kwa kweli tunalaani vikali tukio hili ambalo tunajua chanzo chake ni vuguvugu la uchaguzi ambao, hata hivyo Mahakama na Mufti wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) wameusimamisha hadi Mwezi wa Ramadhani uishe,” alisema Shehe Majid.
Aliomba Serikali iingilie kati kwa kuwachukulia hatua wahusika akiwamo mbunge huyo ambaye anadaiwa kuwania nafasi ya uenyekiti katika uchaguzi ili kunusuru damu ya Waislamu wa msikiti huo kumwagika.
Alisema tayari wamepeleka malalamiko yao dhidi ya Turky kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, Katibu wa Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama na Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Wilson Mukama na kuwataka wamchukulie hatua.
Akizungumza kwa njia ya simu, Turky alikataa kuthibitisha kama alikuwapo msikitini hapo au la na kudai kuwa; “Hatuwezi kuzungumzia watu waongo, kama wao wameitisha mkutano na waandishi wa habari na sisi wakweli tutaitisha wa kwetu.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alithibitisha kutokea kwa mapigano hayo ambapo alisema juzi saa tano usiku, askari Polisi walienda katika msikiti huo na kukuta pande mbili zinabishania uongozi wakati shauri hilo liko mahakamani.
“Majeruhi tuliowathibitisha ni wawili na leo (jana) wamefungua jalada la mashitaka wakimtuhumu huyo mbunge kuhusika na vurugu, lakini siwezi kuzungumzia lolote kuhusu mbunge huyo kwa kuwa askari wangu hawakumuona hadi pale uchunguzi utakapokamilika,” alisema Kamanda Minangi.
Mgogoro wa uchaguzi katika msikiti huo umedumu kwa muda mrefu sasa kwani mara ya mwisho kufanyika ilikuwa mwaka 1993.
Kutokana na hali hiyo, walichaguliwa viongozi wa muda kushika nafasi hizo ambao hata hivyo walienguliwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na sasa ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.

No comments: