WAGOMBEA 'WALIOBEBWA' NA MAKUNDI CCM WATOSWA...

Mary Chatanda
Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa wa Arusha, imepinga uteuzi wa wagombea uongozi wa jumuiya za chama hicho kwa madai ya ‘kubebwa’ na kundi lililopo ndani ya chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda alisema jana kwamba katika wilaya ya Monduli, Halmashauri hiyo imekataa uteuzi wa wagombea wa Umoja wa Vijana (UVCCM) kutokana na uteuzi huo kuwa wa kundi fulani ambalo hakulitaja.
Mbali na Monduli, Chatanda alisema katika wilaya za Longido na Karatu, halmashauri hiyo ilikataa uteuzi wa wagombea katika Jumuiya ya Wazazi kutokana na sababu hizo hizo.
Alifafanua kuwa katika wilaya hizo mbili, majina ya baadhi ya wagombea ambao walionekana kutounga mkono kundi fulani ambalo pia hakuwa tayari kulitaja, yalikatwa.
Katibu huyo ambaye ana msimamo wa kutaka viongozi ndani ya chama kufuata utaratibu na kuacha makundi, alisema baada ya kugundua kasoro hizo, kikao cha Halmashauri kiliagiza vikao husika vya uteuzi katika wilaya hizo kupitia upya na kurekebisha kasoro hizo ndani ya wiki moja.
Alisema baada ya kasoro hizo kurekebishwa, viongozi husika wanapaswa kakabidhi mapendekezo hayo kwa Kamati ya Siasa ya Mkoa iliyokasimiwa madaraka ya kuthibitisha uteuzi huo.
Chatanda alisema katika wilaya tatu zilizobakia, Arusha, Arumeru na Meru, uteuzi wake umekubalika na zitaendelea na uchaguzi wake kuanzia Septemba mosi hadi 5 mwaka huu ili kuwapata viongozi katika nafasi hizo.
Katika nafasi ya uenyekiti wa Mkoa, kikao hicho kilipitisha majina ya wagombea watano ambao walijitokeza kuwania nafasi hiyo.
Mwenyekiti wa CCM anayetetea nafasi yake Onesmo ole Nangole amejitosa tena kutetea nafasi hiyo na atachuana na Mganga Mkuu mstaafu wa Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, Dk Salash Toure.
Wengine wanaowania nafasi hiyo ni Hamis Shaaban, mfanyabiashara Onesmo Metili na aliyepata kuwa Shekhe wa Mkoa wa Arusha, Adam Chora.
Katika nafasi ya Katibu wa Siasa na Uenezi, Lootha Sanare anatetea nafasi hiyo na atachuana na Anna Msuya, Gasper Kishumbua, Isack Capriano na Hagai Kissali.
Nafasi ya Katibu wa Fedha na Uchumi kikao hicho kiliwapitisha Juma Losini, anayetetea nafasi hiyo, Violeth Mfuko, Julius Mungure, Hilal Sood, Metili, Victor Mollel, Julius Laizer na Kissali.
Kikao hicho pia kilibariki wagombea uenyekiti wa wilaya sita za mkoa ambapo katika wilaya ya Arusha kuna wagombea saba na ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) na katika wilaya zingine, wapo 18.
Katika wilaya ya Arumeru, wagombea uenyekiti wako tisa na NEC wanne; Meru uenyekiti kuna wagombea wanane na NEC watano; Monduli uenyekiti wako sita, NEC watatu; Longido uenyekiti watatu, NEC sita; Karatu uenyekiti sita, NEC tisa na Ngorongoro uenyekiti wawili, NEC saba huku mgombea ujumbe wa NEC Taifa wa mkoa kwenda kapu ni mmoja Sylvester Meda.
Chatanda alisema kikao hicho pia kilipitisha uteuzi wa wagombea wa nafasi za ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya na nafasi za ujumbe wa mkutano mkuu wa CCM Wilaya za Arusha, Arumeru, Meru, Karatu, Longido na Monduli.
Katika hatua nyingine, kikao hicho kilipitisha majina mawili ya kuwania nafasi za udiwani katika uchaguzi mdogo kwa kata mbili za Daraja Mbili, Arusha na Bangata, Arumeru baada ya madiwani wao kufariki dunia.
Katika kata ya Daraja Mbili, kikao hicho kilimpitisha Phillip Mushi kugombea, baada ya kupita bila kupingwa wakati kwa kata ya Bangata, kilimbariki Olais Mfere, baada ya kupata kura 977 kati ya 1,158 sawa na asilimia 84.4.
Mfere aliwashinda David Mollel aliyepata kura 154 na Ezekiel Lameck aliyepata kura 27.
Naye Namsembaeli Mduma anaripoti kuwa Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan ‘Zungu’, ameshindwa kurejesha fomu za kugombea uenyekiti wa Taifa katika Umoja wa Wazazi wa Jumuiya ya CCM.
Kutokana na hatua hiyo, Mbunge huyo ameondolewa kwenye orodha ya watakaoshiriki uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba.
Ingawa Zungu alilieleza gazeti hili kuwa hagombei tena, lakini Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Khamis Dadi alidai mbunge huyo hakutoa sababu wala kuwasiliana na uongozi wa Jumuiya hiyo kuhusu uamuzi wake, hadi muda wa kurejesha fomu ulipokwisha saa 10 jioni ya juzi.
Pamoja na Zungu, watu wengine 15 wakiwamo wabunge na wafanyabiashara, walichukua fomu hizo zilizoanza kutolewa Agosti 24, mwaka huu mkoani Dar es Salaam, akiwamo mwanamke mmoja tu, Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata.
Wengine waliochukua fomu ya kugombea nafasi hiyo na kuzirejesha kwa muda uliopangwa ni Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono, Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza na Mbunge wa Chalinze, Said Bwanamdogo.
Wengine ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo kuanzia mwaka 1989 hadi 2006, Abiud Maregesi, John Machemba, Mosha Konrad, William Bocco, Maseke Muhono, Manley Mgata, Dk Muzamil Kalokola, Alfred Mwambeleko, Alphonce Siwale, Salim Chicago na Abdalla Bulembo.
Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo wa masuala ya siasa na oganaizesheni, Ali Haji alisema licha ya muda wa kurejesha fomu katika maeneo yote nchini kumalizika, wanaendelea kupokea taarifa za mikoani kwa nafasi mbalimbali kujua idadi ya watakaochuana katika uchaguzi huo.
"Hao 15 waliozungumziwa ni wa Dar es Salaam pekee kwa sababu taarifa za waliochukua fomu mikoani bado tunazipokea kutoka kwa wenzetu wa huko. Kwa ufupi, wanatupa taarifa za waliorudisha, hakuna anayepokea fomu tena kwa sasa," alisema.

No comments: