Kamanda Liberatus Sabas
Tuhuma za ufisadi katika siasa zimeendelea kukisakama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambapo jana Katibu wa Kata ya Endulen wilayani Ngorongoro, Denis Paulo (33) alikamatwa na Polisi kwa madai ya kutaka kufanya utapeli.
Paulo ambaye ni mtumishi wa chama hicho kinachojinasibu kwa kupiga vita ufisadi, alikamatwa na Polisi Arusha kwa tuhuma za kutaka kutapeli wafanyakazi wawili wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Sh milioni 16.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alithibitisha kukamatwa kwa Katibu huyo na kusema Paulo aliwapigia simu wafanyakazi wawili wa NCAA Agosti 27 saa 6 mchana kwa nia ya kuwatapeli.Alidai kwamba baada ya kupiga simu kwa wafanyakazi hao, Paulo ambaye chama chake kimekuwa kikiituhumu Serikali kwa ufisadi, alijitambulisha kwa jina la David Kagasheki na kudai kuwa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii bila kujua kwamba Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ni Maimuna Tarishi.
Katika kujitambulisha huko kwa mujibu wa madai ya Kamanda Sabas, Paulo alidai kwamba Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki ameunda Tume ya kuchunguza tuhuma zilizofikishwa wizarani dhidi ya Menejimenti ya NCAA na yeye ndiye Mwenyekiti.
Ilidaiwa kuwa Paulo alisema yeye na wajumbe wengine sita wa Tume hiyo wako Arusha na jana wangefika ofisi za Mamlaka hiyo kwa mahojiano zaidi.
Kutokana na umuhimu wake katika Tume hiyo, Kamanda Sabas alidai Paulo aliomba fedha kwa wafanyakazi hao ambao majina yao yamehifadhiwa kwa upelelezi zaidi.
Inadaiwa Paulo aliomba kila mfanyakazi atoe Sh milioni 6 na mwingine Sh milioni 10 ili awasaidie kuzima sakata hilo. Alisema wafanyakazi hao walitoa taarifa Polisi wakaweka mtego na kumkamata Paulo kati ya saa 8 na saa 9 alasiri jijini Arusha na hadi sasa inaendelea kumshikilia kwa mahojiano zaidi.
Katibu wa Chadema, Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa alithibitisha kuwapo tuhuma hizo dhidi ya Paulo na kuelezea kushangazwa na madai hayo, huku akidai kuwa hizo ni mbinu za kukichafua chama na kuahidi kulifuatilia suala hilo kwa kina.
Hivi karibuni bungeni Dodoma, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), alisema baadhi ya wabunge, wakiwamo wa Chadema walihongwa na kampuni za mafuta ili kuhujumu uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Hujuma hizo, zilidaiwa kumlenga Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliackim Maswi ili waondolewe katika nafasi zao.
Viongozi hao walidaiwa kukiuka Sheria ya Ununuzi kwa kuzinyima baadhi ya kampuni fedha za zabuni ya kununua mafuta kwa ajili ya kuendesha mitambo ya kufua umeme, ingawa katika uamuzi huo waliokoa zaidi ya Sh bilioni 6 kila mwezi.
Wakati hali ikiwa hivyo Arusha, jijini Dar es Salaam Jumuiya ya Wazazi ya CCM imeelezea kuchukizwa na mwenendo unaofanywa na Chadema kwa madai kuwa imekuwa ikisababisha uvunjifu wa amani na machafuko ya kisiasa nchini.
Mjumbe wa Baraza Kuu Taifa la CCM kupitia Jumuiya ya Wazazi, Dk Salim Chicago alisema hayo jana wakati akitoa tamko la Jumuiya hiyo kuhusu machafuko yaliyotokea Morogoro juzi.
Alisema Jumuiya hiyo Mkoa wa Dar es Salaam inalaani mauaji yaliyotokea Morogoro baada ya Chadema kukiuka agizo la Jeshi la Polisi kuwataka wasiandamane.
No comments:
Post a Comment