Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda ameagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kumwita Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu kama shahidi wa kwanza katika tuhuma zinazowakabili wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa.
Makinda alitoa agizo hilo jana bungeni baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, alipokuwa akitoa Mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM).
Sendeka katika Mwongozo huo, alisema Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alifanya mkutano na waandishi wa habari katika ofisi ya Kambi ya Upinzani juzi na kutaja wabunge wa CCM ambao alisema walikuwa na mgongano wa maslahi katika kamati hiyo.
Alisema Lissu alituhumu wabunge hao kwa kuwataja majina akiwahusisha kutetea kampuni za mafuta ambazo hazikupewa zabuni na Wizara ya Nishati na Madini.
Kwa mujibu wa maelezo ya Sendeka, Lissu aliwahukumu wabunge hao wa kundi moja kutoka CCM huku akitaka Mbunge wa Chadema achunguzwe.
Alisema yeye alikuwa mmoja wa waliotajwa na Lissu kwa jambo ambalo halina ukweli wowote na kumtaka Spika Makinda, kutoa Mwongozo kuhusu kauli ya Lissu, ambayo ilitolewa katika ofisi ya Kambi ya Upinzani na si ndani ya jengo la Bunge, kama ina kinga ya Bunge.
Mbunge huyo wa Simanjiro, alisema hatawasemea wabunge wengine waliotajwa kwa kuwa na wao wana nafasi ya kulisemea, lakini kama kauli hiyo ina kinga ya mbunge husika kutoshitakiwa, inayolindwa na Katiba na Kanuni za Bunge, atamfikisha Lissu katika vikao vya kamati za Bunge atoe ushahidi ujadiliwe.
Kama kauli hiyo ya Lissu haina kinga, Sendeka alisema yuko tayari kwenda mahakamani ili Lissu aitwe kutoa ushahidi, kwa kuwa ana hakika yote aliyosema dhidi yake hayana chembe ya ukweli.
Akitoa Mwongozo, Spika Makinda alitaka wabunge wawe na subira katika suala hilo lililotokana na tuhuma za wabunge kuhongwa na kampuni za mafuta, ili wawawajibishe viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini.
Tuhuma hizo na nyingine za mgongano wa maslahi zilizokumba wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini na wabunge wengine, zilisababisha Spika Makinda Jumamosi iliyopita, kuivunja kamati hiyo na kuagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kushughulikia hizo tuhuma.
Makinda akifafanua kuhusu Mwongozo huo, alisema Mbunge anakuwa na kinga ya Bunge anapozungumza ndani ya Bunge na katika maeneo yaliyo ndani ya mipaka ya Bunge.
Kutokana na hilo, akaagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kumwita Lissu kuwa shahidi wa kwanza katika mgogoro huo.
Juzi, Lissu alitaja wabunge sita wa CCM waliokuwa wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa, akidai kuwa kwa namna moja au nyingine, walihusika kupokea rushwa kutoka kampuni za mafuta ili kuipigia debe Menejimenti ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Wabunge waliotajwa na Lissu ni Munde Tambwe, Sara Msafiri, Mariam Kisangi wa Viti Maalumu, Mbunge wa Korogwe Mjini, Yusuf Nassir na wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage huku akiwasafisha wabunge watatu wa Chadema walioko kwenye Kamati hiyo kuwa hawahusiki na tuhuma hizo.
Wabunge hao ni wa Ubungo, John Mnyika; wa Mbozi Magharibi, David Silinde na wa Viti Maalumu, Mwanamrisho Abama.
Mgogoro huo ulianza takribani wiki mbili kabla ya kuwasilishwa kwa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, ambapo hoja mbalimbali za kuwawajibisha Waziri Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu Eliakim Maswi, zilitawala.
Hoja kubwa ilikuwa ni tuhuma za viongozi hao kukataa kutoa fedha za kununua mafuta kwa ajili ya mitambo ya kufua umeme wa dharura ya IPTL kwa kampuni za Oryx na Camel Oil zilizokuwa zimepewa zabuni na Tanesco kufanya kazi hiyo.
Badala yake, viongozi hao walitoa fedha kwa kampuni ya Puma Energy iliyokuwa BP zamani, ambayo ilikuwa ikiuza mafuta hayo kwa bei nafuu ya chini ya Sh 1,500 kwa lita tofauti na kampuni zilizoingia mkataba na Tanesco, ambazo zinadaiwa kuuza mafuta hayo kwa Sh 1,800 kwa lita.
Kwa uamuzi huo ambao ilikuwa ikidaiwa ulikiuka Sheria ya Ununuzi, viongozi hao waliokoa Sh bilioni 6 zilizokuwa zipotee, kama kampuni zilizoingia mkataba na Tanesco zingepewa fedha hizo.
Profesa Muhongo alipohitimisha hotuba ya makadirio ya bajeti yake, alisema baadhi ya wabunge wanafanya biashara na Tanesco na kuwaomba waache na wengine waliokuwa wakitetea uongozi wa Tanesco, waache upuuzi.
Katika hatua nyingine, CCM imelaani kauli ya Lissu na kuvitaka vyama vya siasa na wanasiasa kuacha kupotosha umma na kuficha ukweli kuhusu suala la tuhuma za rushwa dhidi ya baadhi ya wabunge kwa misingi ya kisiasa.
Pia chama hicho, kilivitaka vyombo husika vinavyochunguza sakata hilo, kumtumia kama shahidi Lissu baada ya kujitokeza juzi na kutaja baadhi ya wabunge wa CCM na kuwahusisha na tuhuma hizo za rushwa.
Kilibainisha kuwa kwa mujibu wa kanuni na taratibu za kimaadili kilichojiwekea, iwapo mbunge wa chama hicho atabainika kujihusisha na vitendo vya rushwa, atasimamishwa uanachama.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa wameanza kulitumia suala hilo kisiasa na kupotosha ukweli kwa umma.
Alitoa mfano wa wanasiasa hao kuwa mmojawao ni Lissu ambaye juzi alitoa orodha ya majina ya wabunge aliowaita watuhumiwa wa kufanya biashara na Tanesco na kwamba ndio watuhumiwa wa rushwa inayozungumzwa bungeni.
"Cha kushangaza, orodha yake ilikuwa na wabunge wa CCM pekee, wakati wote tunajua kuwa yapo majina ya baadhi ya wabunge wa vyama vingine hasa Chadema yanayotajwa katika orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kwa rushwa hii," alisema Nape.
Alisema juhudi hizo za Lissu na wenzake zinalenga kuficha ukweli na kujaribu kulinda watuhumiwa wa uhalifu unaotokana na chama chake, wakati katika mjadala wa Bunge baadhi ya wabunge walimwomba Spika avunje kamati mbili; ya Mashirika ya Umma na Hesabu za Serikali za Mitaa kutokana na tuhuma za rushwa na viongozi wake ni wapinzani.
Nape alisema sakata hilo la rushwa ni zito na linahusu maslahi ya Watanzania katika suala zima la umeme, hivyo wanaotuhumiwa iwapo watathibitika kweli kuhusika ni sawa na wahujumu uchumi kwa hiyo si vyema sakata hilo likageuzwa kuwa la kisiasa.
Aliwataka wote wenye taarifa akiwamo Lissu kuhusu tuhuma hizo za wabunge kuhusika na rushwa kuwa mashahidi namba moja kwa vyombo vya Dola vinavyoshughulikia uchunguzi wa sakata hilo.
"Nasema hivi, kwa kuwa kuna tatizo la baadhi ya watu kutafuta umaarufu kwenye jambo la msingi, sasa kuna hawa waliojitokeza kutaja majina ya wabunge wanaodai ndio watuhumiwa wa rushwa, wasiishie hapo, wakatoe ushahidi wao na kuvisaidia vyombo husika vya Dola ili wahusika wabainike na kuchukuliwa hatua," alisisitiza Nape.
Akizungumzia hatua za CCM iwapo kweli wabunge wa chama hicho watathibitika kujihusisha na tuhuma hizo za rushwa, Nape alisema wana kanuni zinazopinga vitendo vya rushwa na zinazobainisha wazi kuwa mwanachama yeyote bila kujali cheo chake, akithibitika kuhusika na rushwa, husimamishwa uanachama.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Martine Shigela alisema umoja huo unalaani kitendo cha wabunge kufikia hatua ya kutuhumiwa kujihusisha na rushwa na kuitaka Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kuwachukulia hatua wote watakaothibitika kuhusika.
Kwa upande wake, akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri Mkuu mstaafu Dk John Malecela, alisema haungi mkono suala la tuhuma za rushwa lililojitokeza bungeni na kutaka watuhumiwa wote wakithibitika, wachukuliwe hatua za kisheria.
Aidha, aliitaka kamati iliyoundwa kuchunguza tuhuma hizo ifanye kazi kwa kufuata kanuni na sheria bila kujali wahusika ni wa chama gani.
Alisema Spika Makinda atambue kuwa wananchi wanaangalia na kusikiliza kila kinachoendelea bungeni, hivyo itakuwa aibu kama watuhumiwa hao hawatachukuliwa hatua.
"Endapo kamati hiyo itathibitisha watuhumiwa kuhusika na tuhuma hizo, wachukuliwe hatua za kisheria bila kujali ni akina nani na wa chama gani," alisema Malecela.

No comments:
Post a Comment