BEI YA PETROLI YASHUKA BAADA YA ZAIDI YA MIEZI MIWILI...

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imesema bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli, mafuta ya taa na dizeli nchini zitakazoanzia kutumika leo, zimepungua ikilinganishwa na bei kikomo za mwezi uliopita.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Haruna Masebu kwa vyombo vya habari, kwa sasa lita ya mafuta ya petroli kwa rejareja imepungua kwa Sh 170 sawa na asilimia 7.81, dizeli Sh 98 kwa lita sawa na asilimia 4.81 na mafuta ya taa Sh 102 kwa lita sawa na asilimia 5.05.
Kutokana na punguzo hilo la bei kwa baadhi ya maeneo ikiwamo Dar es Salaam sasa lita ya petroli itauzwa kwa Sh 2,009, dizeli 1,943 na mafuta ya taa 1,926; Arusha petroli Sh 2,093, dizeli 2,027 na mafuta ya taa 2,010 na Dodoma petroli Sh 2,067, dizeli 2,001 na mafuta ya taa 1,984.
"Kupungua huku kwa bei kumetokana na kushuka kwa bei za mafuta katika soko la Dunia ikilinganishwa na toleo lililopita la Julai 4," alisema Masebu.
Alisema bei za mafuta hayo katika soko la dunia zilipungua kwa dola 146.40 kwa tani sawa na asilimia 12.73 kwa petroli, dola 74.12 kwaA tani sawa na asilimia 7.55 dizeli, na dola 75.32 kwa tani sawa na asilimia 7.21 sawa na kwa mafuta ya taa.
Alisema kwa bei za jumla ikilinganishwa na mwezi uliopita kwa mafuta ya petroli imepungua kwa asilimia asilimia 8.09, dizeli imepungua kwa asilimia 4.99 na mafuta ya taa imepungua kwa asilimia 5.24.
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko ambapo Ewura itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta hayo.
"Kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ili mradi bei hizo ziko chini ya bei kikomo kama ilivyokokotolewa na fomula mpya iliyopitishwa na Ewura na ambayo ilichapwa kwenye Gazeti la Serikali namba 454 la Desemba 23," alisema Masebu.
Aliagiza vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei mpya za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika na kusisitiza kuwa ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja na adhabu hutolewa kwa kituo husika.

No comments: