TUME YAUNDWA KUCHUNGUZA KIFO MAANDAMANO YA CHADEMA MORO...

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Nchimbi amesema Mkuu wa Polisi (IGP), Saidi Mwema ameunda timu ya kuchunguza mauaji ya mtu mmoja yaliyofanywa na Polisi Morogoro, wakati wa maandamano ya Chadema.
Akizungumza jana Dar es Salaam Nchimbi alisema maofisa walioko kwenye tume hiyo waliondoka jana makao makuu ya Polisi kwenda Morogoro kwa kazi hiyo.
Nchimbi alikiri polisi kupewa taarifa za kuuawa kwa mtu huyo aliyekutwa akiwa na majeraha meta 300 kutoka maandamano yalikofanyikia.
"Polisi walikwenda eneo hilo na kukuta mwili umeondolewa," alisema Nchimbi na kusisitiza kuwa polisi walipiga marufuku maandamano ya Chadema kutokana na kuendelea kwa Sensa ya Watu na Makazi.
Alitoa sababu nyingine ya kutoruhusu maandamano hayo kuwa muda walioomba ulikuwa wa kazi jambo ambalo alisema si busara kuandamana muda huo kwani kungevuruga shughuli za kiuchumi zinazoendeshwa na watu mbalimbali katika barabara sita walizoomba kupita.
Waziri pia aliitaka Chadema kutii na kuheshimu sheria za nchi, kwani bila kufanya hivyo, Taifa litasambaratika.
Alisema hata kama chama hicho hakiridhiki na uamuzi unaofanywa na ngazi moja ni vema kikafuata utaratibu wa kukata rufaa badala ya kulazimisha kama ilivyotokea Morogoro.
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umelaani vurugu na mauaji hayo na kuomba uchunguzi huru ufanyike haraka kubaini waliohusika na mauaji hayo.
Katibu Mkuu wa UVCCM, Martine Shigela alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mauaji hayo yaliyodaiwa kumkumba kijana muuza magazeti wa eneo la Msamvu, aliyefahamika kama Ally Zona (38).
Shigela alisema ni vema vyombo vinavyohusika vifanye uchunguzi huru utakaobaini wahusika wa mauaji hayo na aina ya silaha iliyotumika.
Aliitupia lawama Chadema kwa kuhusika na mauaji hayo na kwamba kama kuna kiongozi anayemiliki silaha atakuwa amekosa sifa ya umiliki.
"Mkakati wote wa vurugu hizo ulifanywa na Chadema, wana tabia ya kutumia vijana katika matukio mbalimbali yakiwamo maandamano haramu kama hayo yaliyosababisha kushambulia wananchi," alisema Shigella na kuongeza kuwa wana ushahidi kuwa hata Igunga walifanya maandamano wakiwa na silaha.
Alidai wanasikitika kwa Chadema kusema waliohusika na tukio hilo ni polisi, kwani ni jambo la kushangaza kwa askari kuacha kuua wananchi walio kwenye msafara na kukimbilia kuua muuza magazeti ambaye hakuwa kwenye maandamano.
Uongozi wa Chadema umesitisha mikutano yake ya M4C mkoani Iringa kwa siku tano ili kupisha siku saba za sensa iliyoanza Agosti 26.
Kusitishwa kwa mikutano hiyo ambayo ilipangwa kuhamia Iringa baada ya kumalizika Morogoro, kulikubaliwa baada ya mazungumzo ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, Mwema na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa.

Dk Slaa alitoa kauli hiyo mjini hapa jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tathmini ya hitimisho la mikutano hiyo ya siku 18 Morogoro.

Polisi mkoani Iringa imepiga marufuku mikutano yote ya Chadema iliyokuwa ianze jana.  
Pamoja na mikutano ya Chadema, Jeshi hilo pia limepiga marufuku mikutano ya vyama vingine vya siasa ikiwamo CCM ambayo iko kwenye uchaguzi wa ndani ili kutekeleza maagizo ya Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa. 
Chadema walipanga kufanya mkutano mkubwa katika viwanja vya Mwembetogwa, lakini pamoja na baadhi ya wabunge wa chama hicho kusisitiza kuwa wana kibali cha kufanya mkutano huo, walishindwa kupenya kwenye uwanja huo. 
Ilikuwa saa sita mchana wakati Kikosi cha Polisi wa Kuzuia Ghasia (FFU) kilipofika uwanjani hapo na kuamuru watu wote wakiwamo wafanyabiashara ndogo kuondoka eneo hilo. 
Wakiwa na mabomu ya machozi na silaha nyingine za kujihami, FFU na makachero wengine wa Polisi, waliimarisha ulinzi uwanjani na kuhakikisha hakuna mkutano unaofanyika nje ya ofisi ya chama hicho ya Mshindo. 
Katibu wa Chadema Iringa Mjini, Suzan Mgonakulima aliwaambia waandishi wa habari kwa kifupi kwamba mkutano huo na mingine iliyokuwa imepangwa kufanywa wiki hii haitafanyika licha ya kuwa na vibali.  
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda alisema Polisi ilipokea maelekezo kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kuzuia mikutano ya kisiasa mpaka sensa itakapokamilika.

No comments: