Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala
Mkazi wa Ndembezi mjini Shinyanga amepigwa na mumewe hadi kuzirai na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu baada ya kutoa ushirikiano kwa karani wa Sensa ya Watu na Makazi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Evarist Mangala, alisema jana kuwa mwanamke huyo, Esther Zablon (40) alipigwa juzi saa mbili asubuhi baada ya mumewe, Ismail Yahya kupata taarifa kuwa karani wa sensa alifika nyumbani kwao na mkewe kukubali kuhesabiwa na kutoa takwimu za familia yao.Akisimulia, Kamanda Mangala alisema karani huyo alipokwenda nyumbani hapo, mume hakuwapo na kama mkuu wa kaya, Esther akazungumza na kutoa taarifa.
Alisema baada ya mume kurudi nyumbani na kugundua kuwa mkewe alikubali kuhesabiwa, alimshambulia kwa ngumi na mateke na kusababisha mke huyo kupoteza fahamu.
Kutokana na kipigo hicho, kwa mujibu wa Kamanda Mangala, Esther alikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa kwa uchunguzi na matibabu.
"Wakati mwanamke huyo akichukua fomu namba tatu ya Polisi (PF3) kituoni kabla ya kufikishwa hospitalini, huku akilia kuwa sababu ya kipigo ni yeye kukubali kuhesabiwa, jambo ambalo ni kinyume na msimamo wa dini ya mumewe (Uislamu)," alisema Kamanda Mangala.
Hata hivyo, Kamanda alisema Esther alitoroka wodini kwa kuhofia mumewe kukamatwa na hatimaye kufungwa.
Kamanda Mangala alisema Polisi wanaendelea kumtafuta Yahya na akipatikana atafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili.
Katika tukio lingine Polisi mkoani humo inawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kumwua na kumpora mali karani wa sensa, Stanley Mahene (34) baada ya kupokea
malipo yake ya semina ya sensa na kurejea nyumbani katika Kijiji cha Kawe Kata ya Iyenze wilayani Kahama.
Kamanda Mangala alisema Mahene alivamiwa Jumapili saa tatu usiku na watu wasiojulikana wakiwa na silaha za jadi na kumshambulia kwa kumkata mapanga.
Mbali na kumkata mapanga, Kamanda Mangala alisema watuhumiwa hao pia walimchoma mshale shingoni na kusababisha kifo chake.
Katika uvamizi huo, walipora Sh 200,000 alizolipwa posho kwenye semina, simu mbili za mkononi, redio, spika mbili na jenereta.
Alisema baada ya mauaji hayo wananchi kwa kushirikiana na Polisi, walianza msako na kuwakamata watu wawili wakiwa na baiskeli tatu zilizokuwa na mali ya karani huyo ambaye pia ni Mwalimu wa Shule ya Msingi ya Kawe.
Kwa mujibu wa Kamanda Mangala, mmoja wa watu waliokuwa na baiskeli hizo alitoroka lakini wawili, Juma Mayala (38) na Idd Lubala (29), wakazi wa Kawe, walikamatwa na baada ya uchunguzi wa Polisi kukamilika, watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.
Mjini Sumbawanga, mkoani Rukwa, karani wa sensa na Mwenyekiti wa Mtaa wa Kliniki eneo la Mazwi mjini humo, walikurupushwa na mapanga wakizuiwa kuendesha sensa.
Akizungumza jana, Mwenyekiti huyo, Michael Mwampulo ‘Kambwa’, alidai kuitwa na karani aliyemkumbuka kwa jina moja la Maembe, akielezea kuzuiwa kufanya kazi katika nyumba ya Muislamu.
Baada ya kufika, Kambwa alidai mkuu wa kaya alisisitiza kuwa hahesabiwi yeye na familia yake, kwa kuwa walitangaziwa na viongozi wao hivyo na baada ya kuendelea kumshawishi, mkuu huyo wa kaya aliingia ndani na kutoka na panga.
Alidai alipotoka nje aliwafukuza kwa silaha hiyo huku akitoa lugha ya matusi hali iliyowalazimu nao kukimbia wakihofia usalama wao na kwenda kutoa taarifa Polisi.
Wakati hilo likijiri, zipo taarifa kwamba baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu waliandamana jana hadi Polisi Mkoa wakishinikiza kuachiwa huru kwa watu watano wanaodaiwa kuwa viongozi wao waliokuwa wakihojiwa kwa kuhamasisha Waislamu wenzao kukataa kuhesabiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda alisema kikundi hicho kiliondoka baadaye baada ya watu hao (majina yanahifadhiwa) kuhojiwa na Polisi kisha kuachiwa.
Wilayani Longido, baadhi ya makarani walikabiliwa na changamoto kadhaa katika sensa baada ya kutembea umbali mrefu kutoka boma moja hadi lingine huku wakinusurika kudhuriwa na wanyama wakali wakiwamo simba.
Simba hao wanadaiwa kuzagaa kwenye baadhi ya vijiji ambavyo vimepakana na Hifadhi ya Amboseli katika nchi jirani ya Kenya.
Msimamizi wa Sensa wa Kijiji cha Sinya, wilayani humo, Herman Kipuyo alisema tangu kuanza kwa sensa, wamekuwa na wakati mgumu kutokana na hali ya kijiografia
katika baadhi ya vijiji.
Herman alisema kwa sasa hofu kwao ni tishio la simba wanaotoka Kenya kwenda Mlima Kilimanjaro kutafuta malisho.
Mkoani Dodoma wananchi wa Bahi Sokoni wilayani Bahi wameandamana hadi kituo cha Polisi kutoa taarifa kuwa makarani wa sensa hawajapita kuwahesabu.
Walichukua hatua hiyo jana baada ya kauli za viongozi wa wilaya na mkoa kutaka kila mmoja ahesabiwe na atakayeshindwa kufanya hivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Habari kutoka eneo la tukio zilisema baada ya kuona maandamano mmoja wa viongozi wa halmashauri hiyo aliwasiliana na Mkuu wa Wilaya, Betty Mkwasa ambaye alitafuta watu kwenda kuzungumza na wananchi hao na kuwaelimisha kuwa kazi hiyo inaendelea kwa siku saba na kila mmoja atahesabiwa.
No comments:
Post a Comment