JARIDA LASISITIZA NYOTA WA FILAMU YA "HOME ALONE" NI TEJA...


JUU: Macaulay katika filamu ya Home Alone (kushoto) na wakati alipokamatwa kwa tuhuma za kutumia bangi (katikati). KULIA: Macaulay alivyo sasa baada ya kuanza kutumia heroin. CHINI: Macaulay akiwa mwenye afya njema akifurahia jambo na mpenzi wake wkabla ya kuanza matumizi ya dawa za kulevya.
Jarida la National Enquirer limeendelea kushikilia msimamo wa kilichoandikwa kwenye habari yao kwamba Macaulay Culkin amejiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya aina ya heroin na ameathirika kwa kiasi kikubwa na matumizi ya dawa za kuzuia maumivu.
Jarida hilo la Marekani limetuma taarifa kwenye mtandao wake, likimwomba nyota huyo wa zamani wa filamu ya Home Alone, mwenye miaka 31, kuomba msaada wa kitaalamu haraka na kumpa changamoto ya kwenda kupimwa damu.
Hatua hii imekuja kufuatia mwakilishi wa nyota huyo kukanusha taarifa za jarida hilo Jumatano iliyopita ambayo ilichapishwa kwenye ukurasa wa mbele wa jarida hilo ikiwa na kichwa cha habari kinachosomeka: "Macaulay Culkin aathirika na heroin: Ana miezi 6 tu ya kuishi."
Msemaji wa Macaulay hakutoa na maoni zaidi pale alipofuatwa na waandishi jana, zaidi ya kuipuuza taarifa ya Enquirer kwa kusema ni 'uongo' na 'matusi'.
Jarida la Enquirer lilituma taarifa kwenye mtandao wake jana asubuhi iliyosomeka: "Wakati wawakilishi wa Macaulay wakiendelea kukanusha Jarida la ENQUIRER liko sahihi na taarifa ya kina, tuko tayari kugharimia ofa ya kupimwa damu itakayosimamiwa na maabara inayojitegemea."
Iliongeza: "Ushauri wetu kwa Macaulay ni kuomba msaada wa kitaalamu ili kuepuka madhara makubwa kama yaliyowakuta wapendwa wetu nyota kadhaa, akiwamo Whitney Houston ambaye alifariki mapema mwaka huu."
Taarifa ya Enquirer pia imegusia mkasa wa rafiki wa kike wa Macaulay, Elijah Rosello, ambaye alifariki Machi mwaka huu akiwa na miaka 24 kutokana na kujizidishia dozi ya heroin.
Kwenye habari hiyo, jarida limedai Macaulay na Elijah wamekuwa wakitumia dawa hizo pamoja, na kurejea tena katika taarifa ya jana asubuhi.
Iliendelea: "Tunaamini kwamba nyota huyo wa zamani wa utotoni anatakiwa afanye kila analoweza kupata matibabu ambayo anahitaji kwa udi na uvumba kwa sasa na ambayo yangeweza kuokoa maisha yake Elijah Rosello.
"Familia yake imelithibitishia Jarida la ENQUIRER kwamba alikuwa akitumia dawa za kulevya na Macaulay kabla mauti hayajamkuta kutokana na dawa hizo Machi."
Msemaji wa Macaulay, Michelle Bega aliibatiza taarifa hiyo ambayo ilidai Macaulay anatumia Dola za Marekani 6,000 kwa mwezi kwa ajili ya dawa za kulevya, kuwa ni 'za kutunga' na 'matusi' pale alipofuatwa kwa mara ya kwanza na waandishi kutoa maoni yake Jumatano iliyopita.
Jarida hilo lilimtuhumu Macaulay kutumia mara kwa mara heroin na ameathirika kwa kiasi kikubwa kwa matumizi ya dawa za kutuliza maumivu za oxycodone, anazochanganya na heroin.
Jarida hilo liliendelea kudai kuwa nyota huyo wa utotoni ameigeuza nyumba yake iliyoko Manhattan kuwa pango la dawa za kulevya ambako anajidungwa mwenyewe ama na marafiki zake.
Macaulay anafahamika zaidi kwa ushiriki wake kama Kevin McCallister kwenye filamu ya "Home Alone" mwaka 1990 na mwendelezo wake, "Home Alone: Lost In New York".
Pia amecheza filamu kama Uncle Buck, My Girl na Richie Rich.
Lakini maisha yake ya utu uzima yameshindwa kuoana na mafanikio makubwa aliyopata wakati wa siku za utotoni mwake.
Mwaka 2003 alicheza filamu inayohusiana na utumiaji wa dawa za kulevya pamoja na Seth Green inayofahamika kama "Party Monster", wakati filamu yake ya mwisho kucheza ilikuwa mwaka 2007 iliyofahamika kama "Sex And Breakfast".
Siku hizi anaendesha maisha yake kwa kufanya kazi ya u-DJ kwenye klabu mbalimbali za usiku mjini New York.
Dada wa kufikia wa Macaulay, Jennifer Adamson alifariki kutokana na kuzidisha dozi ya dawa za kulevya mwaka 2000.
Mwaka 2004 alikamatwa akishukiwa kutumia bangi na viambatanisho viwili vya jamii hiyo - Alprazolam na Clonazepam, kisha akapatikana na hatia ya mwendelezo wa makosa ya dawa za kulevya. Alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela kwa awamu tatu.

No comments: