Mkazi wa kijiji cha Mubinyange, Ngara, mkoani Kagera, Adam Balekawe (32), anadaiwa kufanya mauaji ya kinyama, kwa kumchoma sindano ya sumu na kumnywesha sumu mtoto wake mwenye umri wa wiki tatu Amani Adam, akihofia kuchekwa na ndugu kwa kuzaa na mwanamke mwenye ulemavu.
Kutokana na tukio hilo la hivi karibuni, Balekawe ametiwa mbaroni na juzi alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ngara kusomewa mashitaka ya mauaji. Hakutakiwa kujibu lolote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji na hivyo kurudishwa rumande.
Ilidaiwa kuwa, kabla ya kukamatwa Kabanga, mpakani mwa Tanzania na Burundi, mshitakiwa alikuwa anakusudia kutorokea nje ya nchi.
Akisimulia tukio hilo nje ya mahakama, mama wa mtoto aliyekufa, Ombeni Paschal (27) alidai kuzaa mtoto huyo kwa njia ya operesheni, baada ya kushindwa kujifungua kwa njia ya kawaida.
Alidai kuwa siku ya tukio mzazi mwenzake huyo alimtembelea saa nne usiku na kumkuta amelala chumbani na mtoto aliyekuwa na afya njema, ambapo alishangaa kumwona amesimama pembeni mwa kitanda akimwangalia.
"Alifika usiku, nilishituka kumwona amesimama pembeni mwa kitanda, nikamsalimia, lakini wakati huo alikuwa akinimulika na tochi ya simu machoni, kisha akaniomba nimpe mtoto ambebe, nikamvisha mtoto nguo za baridi akamchukua na kutoka naye sebuleni,’’ alidai Ombeni na kuongeza:
"Ghafla nilisikia mtoto akilia kwa sauti mara tatu kama vile amepatwa na kitu, nikashituka, wakati nafanya jitihada za kushuka kitandani na hasa ukizingatia hali yangu ya ulemavu niliyonayo hii, akaingia chumbani akimleta mtoto akaniambia nimnyonyeshe, lakini wakati huo mtoto akawa amepanua midomo huku akitokwa na povu mdomoni’’.
Alidai, alipoulizwa kilichomsibu mtoto mpaka kulia hivyo na kutokwa na povu midomoni, alisema hajui, "kisha akachukua Sh 15,000 akanitupia kitandani na kuniambia anakwenda kutafuta chakula, kwa sababu alikuwa hajala.
"Baada ya kunitupia pesa kitandani, aliondoka, nikamchukua mtoto kumnyonyesha akawa hata hawezi kunyonya huku akitokwa na povu na kujiharishia, hali ambayo ilinichanganya na kunifanya nipige kelele za kuomba msaada kwa majirani ambao walifika mara moja chumbani kwangu,’’ alifafanua Ombeni.
Huku akitokwa machozi, Ombeni ambaye ni mlemavu anayetembea kwa magongo, alidai kuwa baada ya majirani kuona hali hiyo ya mtoto walimchukua na kumkimbiza hospitalini, lakini walipofika nje ya nyumba mtoto alikata roho.
"Alikatia roho hapo mlangoni kwa sababu walipoona hali yake ni ya kutisha na hasa mtoto ambaye alikuwa mzima wa afya njema kabisa na hasa siku hiyo ambapo alikuwa akionekana mchangamfu sana, mimi nilikuwa najiandaa ili niwafuate hospitalini lakini ghafla majirani wakarudi ndani wakaniambia mtoto amekufa.
"Nililia sana, wakati huo shingo lake lilikuwa limekakamaa na upande mmoja kubadilika na kuwa mweusi huku midomo ikiwa wazi na kukakamaa,’’ alieleza Ombeni.
Alidai kuwa tangu alipomweleza mwanamume huyo ambaye amekuwa naye kimapenzi kwa miaka mitatu kwamba ana ujauzito, alibadilika tabia huku akimtaka kuutoa ujauzito huo kwa madai kuwa hayuko tayari kuzaa naye mtoto, kwani amekuwa akichekwa na marafiki na ndugu zake kwamba ‘anatembea’ na mlemavu.
Alisema alikataa, lakini siku moja aliugua na kumweleza mwanamume huyo ambaye alikwenda kumnunulia dawa na kumtaka aimeze, na baada ya hapo alizidiwa ghafla na kukimbizwa katika Hospitali ya Murugwanza ambapo ilibainika kuwa alimeza vidonge vya kutoa mimba, hata hivyo alisema madaktari walifanya jitihada za kuhakikisha kwamba wanaokoa maisha yake na ya mtoto tumboni.
Alibainisha kuwa wakati wote wa ujauzito, mwanamume huyo alikuwa akimweleza kwamba ameanza kuchekwa na ndugu na marafiki kwamba amezaa na mlemavu, huku akisisitiza kuwa hawakuwa na makubaliano ya kuzaa mtoto, bali kufanya mapenzi tu.
Daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa mtoto huyo, Dk Raphael Rwezaula alithibitisha kuwa chanzo cha kifo ni sumu, hata hivyo hakutaja aina ya sumu na kueleza kwamba itapelekwa kwenye maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Dar es Salaam kwa ajili ya vipimo ili kubaini aina ya sumu iliyomwua.
Alisema vipimo vimeonesha kwamba sumu hiyo iliingia mwilini kwa mtoto kwa sindano na kunyweshwa.
Kutokana na hali hiyo, Dk Rwezaula alilazimika kukata baadhi ya vipande vya nyama kutoka mwili wa mtoto huyo shingoni na tumboni, na tayari vimepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili kubaini sumu hiyo.
No comments:
Post a Comment