Kiongozi wa Chama cha Walimu, Gratian Mukoba.
Serikali imewahakikishia walimu ambao hawajajihusisha na mgomo na wanaotishiwa na walimu walioamua kugoma, kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vitawalinda.Lakini pia Serikali imesema Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6 ya mwaka 2004 ambayo Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimeitumia kugoma; inampa fursa pia mwajiri kutolazimika kulipa mshahara kwa mtumishi aliyeshiriki mgomo kwa kipindi chote ambacho atakuwa anagoma.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alikiri kupokea taarifa kutoka sehemu mbalimbali nchini kuwa baadhi ya walimu wamegoma na kwamba wanawanyanyasa na kuwapiga walimu wanaotaka kuendelea kufundisha.
Pia alisema Serikali pia imepokea taarifa za walimu hao kuharibu mali za Serikali, jambo ambalo alisema si busara kwa mtu mwenye taaluma ya ualimu kujihusisha na vitendo vinavyokwenda kinyume cha sheria na taratibu kwa maslahi binafsi.
"Nawahadharisha wote wanaojihusisha na vitendo viovu kama kutisha wenzao, kuwapiga, kuwaharibia mali au kwa njia yoyote kuwanyanyasa kwa sababu ya kuwa hawajaunga mkono kugomea kufundisha, kuwa Serikali itachukua hatua kali dhidi yao," alisema Dk Kawambwa.
Alitoa onyo kwa baadhi ya walimu ambao wanashawishi na kutumia wanafunzi katika mgogoro huo kuwa si haki, kwani mgogoro uliopo ni baina ya walimu na Serikali.
Pia aliomba wazazi na walezi wasikubali na wazuie na wakataze watoto wao kutumiwa au kuhusishwa kwenye mgogoro huo ambao utawahatarishia usalama na maisha yao.
Wakati baadhi ya walimu nchini wakitekeleza agizo la CWT kuanza mgomo jana, inadaiwa Rais wa chama hicho, Gratian Mukoba aliendelea na kazi.
Mukoba anayedaiwa kuwa Mkuu wa Sekondari Benjamin Mkapa, inasemekana jana asubuhi alifika shuleni na kusaini ili kuepuka adhabu ya Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki alisema viongozi wa CWT walihudhuria kazini na kuwachuuza wenzao wasihudhurie.
Alisema aliyeitisha mgomo, bila kumtaja jina, alikuwa kazini katika Sekondari ya Benjamin Mkapa na Mweka Hazina wa chama hicho wa Wilaya ya Kinondoni anayefundisha Sekondari ya Jangwani, naye alikuwa kazini ili kukwepa mkono wa Serikali. Mukoba ndiye aliyeitisha mgomo juzi.
Alisema kutokana na hilo, aliagiza wakurugenzi kutoa barua kuanzia leo kwa ambao hawakufika jana kazini na wasiofundisha ili kujieleza na kama walikuwa na udhuru lazima hatua zichukuliwe. Mukoba alipotafutwa kuzungumzia suala hilo simu zake zote hazikupatikana.
Pia alisema baada ya kufanya uchunguzi ikiwa watabainika kukiuka sheria watafukuzwa kazi, huku akiagiza wakuu wa wilaya kukamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria walimu wanaohamasisha migomo kwa kutuma ujumbe mfupi wa simu na kutisha wanaoendelea na kazi.
Alisema pia wapo wanaofika shuleni na kuchochea walimu na kuwasihi viongozi wa CWT kufanya uchochezi nje ya majengo ya Serikali, kwani CWT haina shule.
Akizungumzia kuhusu upigaji kura kwa walimu kuunga mkono mgomo, alisema zaidi ya asilimia 90 ya walimu wa shule ya msingi na sekondari katika mkoa huo hawakushiriki.
Akizungumzia hali ya mgomo, alisema zaidi ya silimia 85 ya walimu wa shule za msingi na asilimia 96 ya wa sekondari walihudhuria shuleni. Alisema mgomo ulikuwepo katika shule za msingi za katika kata nne za Manispaa ya Kinondoni.
Baadhi ya shule za Dar es Salaam zimebainika kuwapo kuwapo kwenye mgomo kama vile Ukombozi ya Manzese iliyokuwa na Mwalimu Mkuu pekee.
No comments:
Post a Comment